Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, wanadaiwa waliingia ‘anga’ za ofisi
za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Bariadi na kusababisha
taharuki kubwa, baada ya
mmoja wa wafuasi wake kudaiwa kufyatua risasi tatu
hewani. Tukio hilo lilitokea katika ofisi za Chadema juzi saa 1:30 jioni baada
ya wafuasi wa Chadema kumsindikiza mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec),
John Heche, aliyetoka kumsindikiza Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho, John
Mnyika, aliyekuwa akienda wilayani Maswa kwa shughuli za kichama.
Msafara wa Chenge ulikuwa ukitokea katika mkutano kwenye
kijiji cha Isanga, na wale wa Chadema wakiwa wamerudi toka mkutano uliofanyika
viwanja vya Basketi mjini hapa, ndipo walipokutana na msafara wa Chenge jirani
na ofisi za Chadema na kuanza mabishano.
Inadaiwa msafara wa Chenge ulisimama katika ofisi hizo
ukiwa na magari matano, huku moja ya magari hayo likipiga muziki kwa sauti
kubwa, hali iliyosababisha wafuasi wa Chadema kuurushia mawe na kuwazomea.
KAULI YA POLISI
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi, alisema vyama hivyo baada ya
kumaliza mikutano yao, Chadema walianza safari ya kuelekea ofisini kwao katika
barabara ya Maswa, huku msafara wa Chenge ukitokea kijiji cha Isanga kurejea
mjini.
Alisema baada ya msafara wa Chenge kufika jirani na ofisi
za Chadema walikutana na kundi kubwa likishangilia, ndipo mbunge huyo
aliposhuka katika gari na kuanza kucheza nao, lakini wakati wafuasi hao
wakiendelea kushangilia, walisikia sauti ikisema rusha mawe iliyosababisha
mbunge huyo kukimbilia ndani ya gari.
Kamanda Mushi alisema baada ya wafuasi hao wa Chadema
kurusha mawe kwa kulishambulia gari la Chenge, ndipo kada wa CCM (jina
tunalihifadhi kwa sasa) alipotumia bastola yake kurusha risasi tatu hewani ili
kuwatanya watu waliokuwa wamezingira msafara huo na watu hao kutawanyika.
Hata hivyo, kamanda huyo hakueleza kama mtu huyo
amekamatwa na kama kuna ganda lolote la risasi ambalo polisi waliliokota.
MASHUHUDA WANENA
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema wafuasi wa
Chadema walianza kurusha mawe ndipo mbunge huyo alipokimbilia ndani ya gari
yake.
“Tulishangaa kuona wafuasi wa vyama hivyo wakianza
kushambuliana kwa mawe baada ya kutokea kwenye mikutano yao ya hadhara na
kufika maeneo hayo,” alisema Mkuba Majaliwa.
VIONGOZI WA CHADEMA
Akizungumzia tukio hilo, John Heche, alisema wafuasi wa
CCM walipita katika ofisi za chama chao na kukutana na viongozi pamoja na
wafuasi waliotoka mkutanoni huku CCM wakipiga muziki, hali ambayo ilisababisha
baadhi ya viongozi kuwazuia kwa madai ya kuwataka kupunguza sauti ya muziki.
“Msafara huo ulifika ofisi ya Chadema baada ya kutoka
katika mikutano yao na ulipofika maeneo ya ofisi zetu walisimamisha magari yao
na kuanza kupiga muziki na wafuasi wao waliteremka kwenye magari yao na kuanza
kucheza hali iliyosababisha wafukuzwe kwa mawe na wafuasi wa chama changu,”
alisema Heche.
VIONGOZI WA CCM
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilayani Bariadi, Sai
Samba, alisema baada ya kufika jirani na ofisi ya Chadema walikuta kundi la
vijana wakiwa wamejipanga barabarani na kuzuia msafara wao kwa kurusha mawe
mbele ya gari la Chenge, hali iliyomlazimu mmoja wa wafuasi wa Chenge kurusha
risasi hewani kwa lengo la kuwatawanya.
Hata hivyo, NIPASHE ilipomtafuta Chenge kwa ajili ya
kuzungumzia tukio hilo, hakupokea simu yake ya mkononi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment