Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma kujibu shtaka la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, David Ngunyale, Wakili wa Serikali, Maryasinta Lazaro, alidai kuwa Mbunge huyo alitenda kosa hilo Agosti Mosi, mwaka 2013, katika Kata ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Wakili huyo alidai kuwa Mbunge huyo alimtolea maneno ya matusi Nyembo kuwa hana maadili, ana akili finyu na ni kiumbe dhaifu, kitendo ambacho kingesababisha uvunjifu wa amani.
Wakili Lazaro, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo namba CC 6/2015 umekamilika na kuomba kupangwa tarehe nyingine ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu Ngunyale alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 19, mwaka huu.
Wakili wa Mbunge huyo, Danieli Rumenyela, aliomba Mahakama hiyo kumpunguzia mteja wake masharti ya dhamana ili kumalizia vikao vya Bunge ambavyo vinatarajia kuanza mwezi ujao.
Hata hivyo, Kafulila alikana shtaka hilo na kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kata na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni mbili kisha kuachiwa.
Kafulila alidhaminiwa na Diwani wa Kata ya Katubuka (Chadema), Moses Bilantanye.
Kabla ya kufikishwa mahakamani jana, Mbunge huyo alikuwa nje kwa dhamana ambayo alipewa na askari wa kituo cha Polisi Kati baada ya kudaiwa kumtukana Mkuu huyo wa wilaya.
Jana Kafulila aliporipoti katika kituo hicho saa 1:00 asubuhi, alipelekwa mahakamani hapo baada ya Mwanasheria wa Serikali kuandaa mashtaka dhidi yake.
HALI ILIVYOKUWA
Nje ya mahakama hiyo walifurika wafuasi wa vyama vya siasa vya upinzani wakiwamo madiwani, wapambe wa mbunge huyo ambaye ndiye aliyeibua bungeni sakata la uchotaji wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Pia ulinzi ulikuwa umeimarishwa katika Mahakama hiyo, ambako pia kulikuwa na usikilizaji wa kesi za mauaji zilizokuwa zinasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment