CHAMA cha Wananchi (CUF) kimekubaliana na uamuzi wa
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi wa kukifuta katika orodha ya
vyama vya siasa kwa sababu hakiko tayari kuvunja vikundi vyake vya ulinzi
vinavyojulikana kwa majina ya Blue Guard na White Guard.
Kimesema kwa sasa licha ya kuwepo zuio la kuvitumia
vikundi hivyo kutoka kwa Jaji Mutungi na Mkuu wa Jeshi la wa Polisi (IGP),
Ernest Mangu, kitaendelea kuvitumia vikundi hivyo katika ziara zake za kichama
zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni katika mikoa ya Kusini, Kanda ya Kati na
Kanda ya Ziwa.
Uamuzi huo wa CUF umetolewa jana na Mkurugenzi wa Uenezi,
Abdual Kambaya katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyikia makao
makuu ya chama hicho.
Kambaya ametangaza msimamo huo ikiwa ni siku chache baada
ya Jaji Mutungi kupiga marufuku vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama,
kwa kile alichoeleza kuwa kwa sababu uwepo wake ni kinyume cha Katiba ya
Jamhuri ya Muungano inayotoa jukumu la ulinzi na usalama wa raia na mali zao
kwa Jeshi la Polisi.
Jaji Mutungi alitoa agizo la kufutwa kwa vikundi hivyo
katika mkutano wake na vyama vya siasa pamoja na Jeshi la Polisi, kwa kuvitaka
vyama vya siasa ambavyo Katiba zake zinatambua uwepo wa vyama hivyo,
virekebishe kwa kuviondoa kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, Kambaya alisema agizo hilo la Jaji Mutungi
halitekelezeki kwa sababu vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vipo kwa
mujibu wa sheria na Katiba inavitambua na hata ofisi ya msajili ya vyama ina
taarifa za uwepo wake.
Kambaya alisema iwapo Ofisi ya Msajili imedhamiria
kusimamia agizo lake hilo inapaswa kukipatia CUF Sh bilioni moja ambacho ndicho
kiasi kinachohitajika kwa ajili ya kuitisha mkutano mkuu utakaoamua kufutwa kwa
vikosi hivyo.
“CUF tunaona kauli za msajili wa vyama vya siasa na IGP
Ernest Mangu ni za kuchekesha kwa sababu wanachokitaka hakiwezekani, vikundi
hivi vipo kisheria na Katiba ya nchi inavitambua.
“Kama kweli Jaji Mutungi anamaanisha anachokisema, basi
utaratibu wetu wa kufanya hivyo anaujua kwani Katiba ya chama inarekebishwa na
wanachama kupitia mkutano mkuu wa taifa, hivyo atupatie bilioni moja ambayo ni
bajeti yetu ya kuitisha mkutano huo,” alisema Kambaya.
Akizungumzia majukumu ya vikundi hivyo alisema havipo kwa
ajili ya kupambana na polisi, bali kulisaidia kufanikisha kazi ya usalama wa
raia kwa sababu limeshindwa kufanya kazi kwa ufanisi hasa katika shughuli za
kisiasa.
“Iwapo IGP anataka kushughulikia vikosi vya ulinzi na
usalama aanze na vile vya kigaidi na uhalifu wakati wa uchaguzi vinavyomilikiwa
na CCM kama vile vya Janjaweed na GreenGuard na Chinjachinja, ambavyo ni
maarufu kwa kufanya uhalifu,” alisema Kambaya.
Alisema chama chake kitavitumia vikundi vyake vya ulinzi
na usalama katika ziara kinazokusudia kuzifanya hivi karibuni kwenye mikoa ya
Kanda ya Kusini zitakazoongozwa na Mwenyekiti wa Chama, Profesa Ibrahim Lipumba
na mikoa mingine kuanzia Dodoma itaongozwa na Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi
na Bunge, Shaweji Mketo.
Aidha, Kambaya alisema Tume ya Uchaguzi imehodhi mchakato
wa kutoa elimu kuhusu kura ya maoni ambao ulipaswa kutekelezwa na asasi za
kiraia (NGOs).
Msimamo huu wa CUF unafanana kwa kiwango kikubwa na ule
uliotolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe aliyesema kuwa litakuwa jambo la kiuwendawazimu kuvifuta vikundi
hivyo.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment