Wednesday, April 22, 2015

Watanzania waliokuwa wakiishi Yemen wakarejea nchini kutokana na machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo waelezea mateso yao

SERIKALI imefanikisha kurejea nchini kwa kundi la pili la Watanzania 14 wanaoishi Yemen, ambako kuna machafuko ya vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Watu hao wameelezea jinsi walivyoteseka
na kuathirika kisaikolojia, huku wakiwataka Watanzania waliopo nchini, kutojaribu kuichezea amani iliyopo.

Katika kuyanusuru maisha yao, Watanzania hao waliogharamia chakula, malazi na usafiri wa kurejea nchini, wamesema walilazimika kutangatanga kwa zaidi ya wiki mbili na hatimaye kufanikiwa kurejea salama nchini.

Kurejea kwao jana, kumefanya watanzania waliorejea nchini hadi sasa kutoka Yemen kufikia 39, kati ya 64 waliopo nchini humo.

Wakizungumza na HABARI LEO jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam baada ya kurejea na ndege ya Shirika la Ndege ya Emirates yenye namba EK 725, watanzania hao walisema kama sio juhudi za serikali ya Tanzania, wana uhakika kwa sasa wangekuwa wafu.

“Sina cha kusema, kwa kweli naishukuru serikali yangu na Balozi wangu kule Muscat, Oman alitusaidia sana, nilikuwa naishi Yemen mimi na familia yangu ya watu 10, na hali ilipozidi kuwa mbaya niliomba msaada ubalozini na walitusaidia na tumerejea nyumbani na familia yangu kwa gharama za serikali, hili sio jambo dogo,”alisema Sabri Abeid Almaghi.

Akisimulia hali halisi nchini Yemen, Almaghi alisema tangu mwaka 2011 amekuwa akiishi nchini humo yeye na mkewe na familia yake ya watu 10, akifanya biashara ya maduka ya kuuza vipuri vya pikipiki na kwamba hali ya siasa ikachafuka na mapigano yakaanza.

Alisema baada ya machafuko kutokea, ilimbidi afunge maduka yake na kuhamishia vipuri vyote kwenye stoo moja na kisha kurudisha maduka ya watu aliyokuwa amepanga na kuanza kutafuta msaada ubalozini wa kurejea nyumbani.

“Kwa kweli kule hivi sasa ni taabu tupu, hali sio nzuri kwanza uwanja wa ndege ulifungwa, tukaambiwa muda unavyokwenda barabara nazo zitafungwa, nilikuwa ninaishi mji uitwao Mukalla, baada ya kuona hali mbaya nilipiga simu ubalozini, kuomba msaada na ndipo tukaanza safari ya kuondoka Yemen kwa basi kwenda Muscat, tumechukua zaidi ya siku tano kusafiri,”alisema Almaghi.

Aliongeza kuwa, kwa ujumla tangu walipoanza safari ya kuondoka Yemen hadi kufika Tanzania wakiwa salama jana, wametumia zaidi ya siku 15, jambo ambalo aliloelezea kuwa limempa uchovu mkubwa hasa kwa kuwa alikuwa na watoto na watu wengine wa familia yake.

Akiendelea kusimulia jinsi yeye na familia yake walivyoondoka salama Yemen, Almaghi alisema baada ya kutoa taarifa kwenye ubalozi wa Tanzania nchini Oman, Balozi Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini humo alichukua hatua za dharura kuwanusuru na kuhakikisha wanaingia nchini Oman.

Alisema gharama za kutoka mji waliokuwa kufika Oman zilikuwa juu yao, ila baada ya kufika Oman serikali ya Tanzania iliwagharamia mahitaji yote hadi kuwapatia tiketi za ndege kwa familia yote kurejea nyumbani. “Kwa kweli nimshukuru Rais Jakaya Kikwete na serikali yake, na pia namshukuru Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe kwa kutusaidia tumerejea salama, ingawa tuna uchovu ila tuko salama nyumbani”, alisema Almaghi.

Naye Saleh Mbarhka Jabri, alishindwa kuzuia hisia zake za furaha baada ya kufika Tanzania hiyo jana akiwa miongoni mwa watanzania 14 waliorejea. “Jamani tuendelee kuomba amani Tanzania, nchi za wenzetu hali ni mbaya usiichezee amani tuliyo nayo,” alisema kwa hisia kali Jabri.

Alisema kama si Serikali ya Tanzania angekuwa ameshakufa kwenye machafuko hayo, kwa sababu hali ni mbaya kwenye miji mingi na kwamba alikwenda nchini humo kuwajulia hali watoto wake na machafuko hayo yakamkuta.

“Niwaase Watanzania wenzangu, tuendelee kuitunza amani yetu na mshikamano wetu, hali siyo nzuri Yemen, niishukuru nchi yangu kwa kutujali tumerejea salama kwa gharama za serikali, hatuna cha kusema zaidi ya kushukuru,”alisema Jabri.

Kwa upande wake, Abdulwahid Said Omary, Mtanzania mfanyabiashara wa Comoro aliyekuwa nchini Yemen, alisema machafuko nchini Yemen ni makubwa, na watanzania wanapaswa kudumisha amani na kamwe wasithubutu kuichezea.

“Tuendelee kuiombea nchi yetu, tuna amani, serikali yangu naishukuru nimerejea nyumbani salama, ingawa mke wangu nimemuacha Yemen kwenye mji salama kidogo kwa kuwa hali yake ya ujauzito hakuruhusiwa kusafiri, anatarajia kujifungua muda wowote,” alisema Omary.

Alisema yeye hufanya biashara kati ya Yemen, Comoro na Tanzania na kwamba machafuko yalimkuta akiwa Yemen siku nne kabla ya safari yake ya kuelekea Comoro, na alipoulizia ndege yake kuhusu safari, aliambiwa uwanja umefungwa.

‘Kwa kweli hapo nikawa sina jinsi, mke wangu na mimi tuliondoka kwenye mji wenye machafuko na kupata hifadhi kwa mama mmoja wa Comoro kwenye mji wa mpakani, hadi hapo nilipoomba msaada kwenye ubalozi wangu wa Tanzania mjini Muscat, Oman na kutusaidia, na leo(jana) tumerejea salama na watanzania wengine,”alisema Omary.

Akizungumzia hatma ya mkewe na biashara zake, Omary alisema hali itakaporejea shwari atarudi kumchukua mkewe, lakini kwa sasa hawezi kwa kuwa hali sio nzuri na kuwasisitiza watanzania kuendelea kuitunza amani iliyopo nchini.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini, Mindi Kasiga, aliyekuwepo uwanjani hapo na maofisa wengine wa wizara hiyo, alisema awamu ya tatu ya watanzania itarejea wakati wowote baada ya ubalozi wa Tanzania mjini Muscat, kukamilisha taratibu za safari zao.

No comments:

Post a Comment