Mwili wa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya
Sekondari Matui wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, Noel Bichima aliyefariki dunia
kwa madai ya kuchapwa viboko na mwalimu wake, umezikwa jana kwenye Kijiji cha
Matui.
Akizungumza kabla ya mazishi, Mchungaji wa Kanisa la
Anglikana, Parishi ya Malamka, Julius Matakala aliwataka wananchi wakubaliane
na hali iliyotokea na wawe tayari muda wote kwa kuwa ni marehemu watarajiwa.
“Tunaiomba Serikali iangalie namna ya walimu wanavyotoa
adhabu, lazima wafuate vigezo, kifo hicho kimesababishwa na uzembe ila watu
waendelee kumuabudu Mungu kila mmoja na imani yake kwa kuwa hatujui siku wala
saa,” alisema.
Wananchi waliokuwapo msibani hapo, walisikitishwa na
kitendo hicho cha mwanafunzi kuchapwa hadi kufariki dunia, wakisema huo ni
ukatili.
Hata hivyo, walisema wameliridhishwa na Serikali
kuwakamata walimu watatu wanaodaiwa kusababisha kifo hicho.
Mjomba wa marehemu, Michael Mtwite akizungumza wakati wa
mazishi alisema wameshafanya uchunguzi kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma na wanasubiri majibu.
“Lakini hatuhitaji uchunguzi sana kwa sababu viboko ndiyo
vimesababisha kifo chake, viongozi wa Kiteto waangalie adhabu zinazotolewa
shuleni na ziwe na viwango ili tukio kama hili lisitokee tena,” alisema Mtite.
Mwanafunzi huyo alifariki dunia kwa madai ya kuchapwa
viboko zaidi ya 12 na walimu watatu wa shule hiyo Aprili 20, saa nne asubuhi
baada ya kufeli mtihani wa Kiswahili kwa kupata alama 40.
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Samwel Nzoka alisema
walimu watatu wanashikiliwa na polisi wakidaiwa kusababisha kifo hicho.
“Mwalimu Peter Bajuta anadaiwa kumchapa viboko vinane,
mwalimu Joyce Makongoro na mwalimu Sheila Ngereza wote kwa pamoja wanadaiwa
kumchapa viboko viwili kila mmoja,” alisema.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment