Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam,
imemwachia huru Mbunge wa Bahi, mkoani Dodoma, Omary Badwel, (pichani) baada ya
upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen
Riwa na kusema mahakama baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa
Jamhuri imeona bila kuacha shaka mshtakiwa hana hatia, hivyo inamuachia huru.
“Mahakama hii imeona ushahidi uliotolewa na Jamhuri
mshtakiwa huna hatia na kwamba inakuachia huru… inawezekana kweli uliomba na
kupokea rushwa lakini kwa ushahidi uliotolewa hauna mashiko ya kisheria wa
kuweza kukutia hatiani, “ alisema na kuongeza:
“Kwa kuwa ushahidi haujathibitisha mashitaka yaliyokuwa
mbele ya mahakama hii na kama unaingilia maslahi, mali na maisha ya watu huko
jimboni kwako uache endelea kufanya mambo yako ya kisiasa.”
Alisema kwa mujibu wa ushahidi wa mazungumzo
yaliyorekodiwa na wakati wa tukio uliotolewa mahakamani, sauti ya mshtakiwa
haikusikika akiomba wala kushawishi rushwa, lakini amesikika aliyekuwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Sipora Liana.
Alisema pamoja na mambo mengine, mshtakiwa ana wadhifa
mkubwa na kwamba siyo rahisi yeye na kamati yote kuomba rushwa yenye thamani ya
Sh. milioni moja kwa kila mjumbe.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa mshtakiwa akiwa kama Mbunge wa Jimbo hilo,
Mjumbe LAAC na mtumishi wa umma, alitenda kosa hilo kati ya Mei 30 hadi Juni 2,
mwaka 2012 jijini Dar es Salaam.
Ilidaiwa kuwa
kinyume cha Sheria ya Kupambana na Kuzuia Rushwa, Mbunge huyo
alishawishi kutolewa kwa rushwa ya Sh.
milioni 8 kutoka kwa Liana ili awashawishi wajumbe wa kamati hiyo wakati wa
kupitia ripoti ya bajeti ya halmashauri hiyo ya mwaka 2011/12.
Ilidaiwa katika shitaka la pili kuwa, Juni 2, mwaka 2012,
katika Hotel ya Peacock, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alipokea rushwa ya
Sh. milioni moja kutoka kwa Liana kwa ajili ya kuwashawishi wajumbe wa LAAC
kupitisha ripoti ya bajeti ya halmashauri hiyo ya mwaka 2011/12 bila vikwazo.
Hata hivyo, Mbunge huyo alikana mashtaka dhidi yake na alikuwa nje kwa dhamana.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment