IKULU imesema Rais Jakaya Kikwete atasaini Muswada wa
Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kwa kuwa umepitia taratibu zote.
Pia, Ikulu imesisitiza kuwa sheria hiyo ni nzuri na itadhibiti matumizi mabaya
ya mtandao.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu
alitoa taarifa hiyo
jana, alipozungumza na waandishi wa habari, Ikulu jijini
Dar es Salaam. Rweyemamu alisema sheria ya Makosa ya Mtandao itasainiwa na rais
muda wowote.
“Hii ni sheria nzuri, kwanza inadhibiti matumizi
mabaya ya mitandao, wote watakaohusishwa ama kutuma au kutumiwa vitu au picha
mbaya sheria itawabana wote, na kama umetumiwa bila idhini yako, toa taarifa
polisi, ili uwe kwenye upande salama,” alisema Rweyemamu.
Alisema madai ya wadau kwamba inanyima uhuru wa
kupata taarifa, hayako sahihi kwa kuwa hiyo si sheria ya habari. Alisema
kutokuwa na sheria hiyo, si jambo jema kwa usalama wa nchi.
Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao
ulipitishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge, uliofanyika Dodoma hivi karibuni.
Katika mjadala, wabunge wengi walikemea vitendo vilivyokithiri vya uhalifu wa
mtandao nchini, na kutaka sheria hiyo itakaposainiwa, itumike ipasavyo
kudhibiti.
Wabunge wengi walisema viongozi, watu maarufu na
jamii kwa ujumla, wamekuwa waathirika wakubwa wa matumizi hayo mabaya ya
mtandao, kutokana na kutukanwa, kutishiwa kuuawa, kuzushiwa uongo na hata
wakati mwingine kutapeliwa.
Hata hivyo, baada ya kupitishwa muswada huo,
kumekuwapo na kauli za ukosoaji kutoka kwa watu binafsi na makundi mbalimbali,
wakitaka rais asisaini hadi baadhi ya vifungu virekebishwe.
Miongoni mwa mambo yaliyokosolewa ni pamoja na
sheria kubana pia mtu anayetumiwa vitu au picha mbaya . Wakati huo huo,
Rweyemamu akizungumzia Muswada wa Sheria ya Takwimu kuhusu maombi ya wadau ya
kutaka ziangaliwe pande zote mbili wakati wa kutiwa hatiani, kutokana na kutoa
au kuandika takwimu zisizo sahihi. Alisema maombi hayo yatazingatiwa.
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Habari, uliopelekwa
pia katika mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni, Rweyemamu alisema “Mimi
naomba wadau wa habari wauunge mkono muswada huu, madai kuwa umepelekwa bungeni
chini ya hati ya dharura sio kosa, na pia madai kuwa haujajadiliwa na wadau
nalo sio sahihi, kwani muswada huu umejadiliwa zaidi ya miaka 10, na mimi pia
nilishiriki kwenye moja ya mkutano wa wadau kuujadili miaka hiyo pale
Morogoro.”
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment