RAIS Kikwete ametunuku watu 42 nishani akiwamo
askari wa kike, Koplo Laura Mushi (32) kwa ushupavu alioonesha baada ya
kupambana na kujiokoa dhidi ya majambazi waliomvamia hivi karibuni katika kituo
cha ulinzi Mikumi, Morogoro.
Askari huyo alitunukiwa nishani sanjari na
viongozi mbalimbali wakiwemo wastaafu, katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja
vya Ikulu jijini Dar es Salaam, ikiwa ni nishani ya kumbukumbu ya Miaka 50 ya
Muungano.
Vile vile, Rais Kikwete alimtunuku Jumanne Ngoma
nishani kwa ugunduzi wa madini ya tanzanite. Ngoma alikuwa mtunukiwa pekee
katika kundi la wananchi wazalendo, ambao kwa vitendo na tabia wameipatia sifa
na heshima kubwa Jamhuri ya Muungano.
Askari shupavu Askari huyo alitunukiwa nishani
ya ushupavu kwa kuelezewa kwamba, alivamiwa na watu hao waliosadikiwa kuwa
majambazi ambao walimfunga kamba shingoni na kuanza kumburuza kuelekea
porini.
Katika maelezo yaliyosomwa kabla ya Rais Kikwete
kumtunuku nishani, ilielezwa kwamba Machi 14 mwaka huu, saa 7:56 usiku akiwa
katika kituo cha ulinzi na silaha aina ya sub machine gun ikiwa na risasi 30
ndani yake, alivamiwa na watu wasiojulikana.
Walimkaba shingoni kwa kamba na kuanza kumburuza
kuelekea eneo la pori lililoko karibu na kituo hicho cha ulinzi. Wakati
anaburuzwa kwa lengo la kumuua na kumnyang’anya silaha aliyokuwa nayo,
alijitahidi kuzuia kamba hiyo ili aendelee kupumua wakati huo huo akidhibiti
asipokonywe silaha hiyo.
“Ukiwa katika hali hiyo ya kukabwa shingo,
uliweza kufungua usalama wa bunduki uliyokuwa nayo na kupiga risasi nne. Hali
hiyo ilisababisha wahalifu hao kuacha kukuburuza na wakakimbia kusikojulikana,”
alisema……. “Kitendo ulichofanya kilikuwa ni cha kishupavu na kizalendo na
kiliwezesha kuokoa maisha yako pamoja na silaha hiyo.
Aidha kitendo hicho kimeleta heshima kubwa kwa
jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania na taifa kwa ujumla. Kwa kutambua
kitendo hicho cha kishupavu, mimi Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nakutunuku nishani ya ushupavu”.
Kwa mujibu wa wasifu uliosomwa kabla ya Rais
Kikwete kumtunuku nishani, askari huyo alizaliwa Agosti 23 katika Kata ya
Kimangeni tarafa ya Kifumbu, wilaya ya Moshi Vijijini mkoani
Kilimanjaro.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya Okeseni
iliyoko Moshi Vijijini kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1997 na ya Sekondari
katika shule ya Shimbwe kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2001.
Alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka
2003 na kufanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili. Mwaka 2007 alijiunga na
JWTZ.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment