MAMILIONI ya shilingi yanadaiwa kutumika katika sherehe
ya kuadhimisha miaka 70 ya kuzaliwa kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya VIP
Engineering, iliyokuwa ikimiliki hisa za mitambo ya kufua umeme ya IPTL, James
Rugemalira.
Shughuli hiyo inayodaiwa kufanyika nyumbani kwa mtoto
wake aitwaye Eve, eneo la Makongo Juu, jijini Dar es Salaam katikati ya wiki
iliyopita, iliwakusanya watu wasiopungua 70, wakiwemo watoto wake, wajukuu na
baadhi ya marafiki wa familia hiyo.
Habari ambazo MTANZANIA Jumamosi imedokezwa, zinaeleza
kuwa mamilioni hayo ya fedha yametumika zaidi katika vinywaji baridi na pombe
kali, chakula na mapambo ambayo peke yake yamegharimu shilingi milioni nane.
Taarifa hizo pia zimethibitishwa kupitia picha
zilizowekwa katika akaunti ya mtandao wa kijamii wa Instagram inayomilikiwa na
mtoto wa Rugemalira, Eve, maarufu kama Eve Collections, ambazo zimetoa taswira
halisi jinsi sherehe hiyo ilivyokuwa ya kufana.
Hata hivyo, haijajulikana mara moja kiasi alichotoa
Rugemalira kwa ajili ya kufanikisha shughuli hiyo, lakini mtoto wake huyo, Eve,
aliandika akidai kuwa yeye ndiye aliyeandaa sherehe hiyo.
Juhudi za kumpata Rugemalira, mwanafamilia yeyote au Eve
mwenyewe kwa ajili ya kuzungumzia kumbukumbu hiyo kwa siku ya jana
zilishindikana kutokana na kuwa kwenye shughuli nyingine ya kumbukumbu ya kifo
cha mtoto wake aitwaye Isabela.
Katika siku za hivi karibuni, jina la Rugemalira
limegeuka kuwa gumzo katika vyombo mbalimbali vya habari kutokana na kuhusishwa
katika sakata la fedha zilizochotwa katika akaunti ya Escrow, ambazo kimsingi
zilihifadhiwa baada ya kuwapo mgogoro wa malipo kati ya IPTL na mteja wake wa
nishati ya umeme, Tanesco.
Rugemalira, ambaye anadaiwa kupata shilingi bilioni 130
kama mgawo wake wa fedha hizo za Escrow baada ya kuuza hisa asilimia 30
alizokuwa akizimiliki kupitia kampuni yake ya VIP Engineering, kutajwa kwake
katika sakata hili la Escrow, kunatokana na umahiri wake wa kugawa kiasi cha
fedha hizo kwa watu mbalimbali, wakiwemo wabunge na baadhi ya watumishi wa
umma, hatua ambayo imeibua maswali mengi.
Mgawo wake huo tayari umewaweka watu kadhaa matatani, akiwemo
aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka,
aliyempatia kiasi cha Sh bilioni 1.6 kupitia Benki ya Mkombozi.
Profesa Tibaijuka alifutwa kazi na Rais Jakaya Kikwete
baada ya kukiri kupokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Rugemalira.
Wengine waliokumbwa na kadhia ya kupokea fedha kutoka kwa
Rugemalira na sasa wamekutana na mkono wa sheria ni aliyekuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge (Sh bil 1.6), Mwenyekiti wa Kamati ya
Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na
Sheria, William Ngeleja (Sh mil 40.4).
Rugemalira mwenyewe, akijiita ‘Father James’ amekataa
kutoa maelezo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rusha (Takukuru), akisema kuwa
fedha hizo ni zake, hivyo kuhoji wanachomtafutia.
Hatua yake hiyo inadaiwa kuleta shida kisheria, kwani
amekuwa akisisitiza kufikishwa mahakamani na si kuhojiwa na Takukuru.
Rugemalira, ambaye anatajwa kuwa na ukwasi mkubwa, katika
sherehe yake hiyo ya kuadhimisha miaka 70 tangu azaliwe, kwa jinsi
ilivyoonekana kufana maandalizi yake unaweza kuyalinganisha na harusi za watu
wa hadhi ya kati ambazo mara nyingi gharama yake ni kati ya milioni 20-50.
Kadi za mwaliko
Wageni waalikwa waliofika katika hafla hiyo walitakiwa
kupita katika meza maalumu iliyokuwa na kadi maalumu zenye jina la Rugemalira,
lakini pia na majina yao (wageni waalikwa) na zilikuwa zikiwaelekeza meza
wanayotakiwa kukaa.
Mapambo
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa eneo
ilipofanyika hafla hiyo lilipambwa kwa maua mengi halisi ya rose na mengine
mengi ya gharama ya juu, huku kukiwa na mishumaa mizuri ya kutosha iliyoongeza
mng’ao wa kipekee ambapo mmoja wa watu wa karibu aliliambia gazeti hili kuwa
gharama za mapambo pekee zinaweza kufikia Sh milioni nane.
Mwandaaji wa hafla hiyo, ambaye ni mtoto wa Rugemalira,
Eve, aliyejaaliwa kipaji cha ubunifu, hasa wa mavazi ya kike, aliandika katika
akaunti yake hiyo ya Instagram kwamba mapambo ya ndani yaliyonogeshwa na
mishumaa mingi yamefanya eneo hilo kuwa na mwonekano tofauti kabisa.
Ukumbi pia ulinogeshwa na mapambo ya rangi tofauti
tofauti, lakini rangi kuu iliyobeba shughuli hiyo ilikuwa ya bluu, ambayo
ilibebwa zaidi kwenye vitambaa vilivyotandikwa mezani na ‘napkin’ zilizowekwa
kwa ajili ya wageni waalikwa kuzitumia wakati wa chakula.
Vyakula
Vyakula vingi vilikuwa vya kukaanga, vikiwa katika aina
tofauti tofauti, baadhi yake ikiwa ni kuku, ndizi, na samaki aina ya kamba.
Vingine ni wali, mboga za majani na vingine vingi, huku
vikienda na vinywaji mbalimbali, ikiwemo bia aina ya Windhoek iliyowekwa sehemu
maalumu na kuelezewa kama kinywaji pendwa cha mzee Rugemalira.
Inadaiwa kuwa vyakula hivyo vilivyoandaliwa na
Dorkacatering vilikuwa maalumu kutokana na umuhimu wake, kwani sahani moja ya
chakula iligharimu kiasi cha Sh 30,000.
Keki
Ukiacha keki kuu ya shughuli iliyokuwa na ngazi tatu na
iliyokuwa imezungukwa na mishumaa, kulikuwa na keki nyingine nyingi zilizowekwa
meza kuu na meza nyingine maalumu.
Wageni waalikwa
Mbali na wanafamilia ambao ni watoto, wajukuu, baadhi ya marafiki
wa familia hiyo, akiwemo Ritha Paulsen, maarufu kama Madam Ritha, alialikwa
kuhudhuria hafla hiyo ya kipekee ambapo pia walipata muda mzuri wa kula na
kucheza ukumbini hapo.
Mbali na kuandaa hafla hiyo, Eve alimshukuru Mungu kwa
kumuweka baba yao hai mpaka wakati huu ambao wanasherehekea miaka 70 ya uhai
wake wakiwa naye.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment