WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowasa, jana alithibitisha
kwa vitendo kuwa afya yake iko safi baada ya kutembea umbali wa kilomita tano
kwa miguu kwenye matembezi ya kupinga mauaji ya albino nchini.
Kwa muda mrefu, Lowassa ambaye ni mmoja wa makada wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi
mkuu wa Oktoba mwaka huu, amekuwa akidaiwa kuwa na matatizo ya afya na kuwa
hawezi kuhimili mikimiki ya kampeni na shughuli nyingine zinazohitaji nguvu.
Lakini matembezi ya jana yaliyoongozwa na Lowassa kuanzia
Uwanja wa Taifa wilayani Temeke mpaka viwanja vya TCC Chan’gombe na kutumia
dakika 25, yamedhihirisha vinginevyo.
Matembezi hayo yalianzia barabara ya Mandela, Kilwa
kupitia Temeke Mwisho, Wiles, Temeke Hospitali, Chang’ombe Polisi, Kiwanda cha
Bia cha Serengeti na kuhitimishiwa viwanja vya TCC.
Akizungumza baada ya kuhitimisha matembezi hayo
yaliyoandaliwa na kikundi cha Temeke Family Sport Club, Lowassa alisema
hakushiriki matembezi hayo kwa lengo la kufanya siasa bali ni kumuunga mkono
Rais Jakaya Kikwete katika vita dhidi ya mauaji ya albino.
“Hapa sikuja kufanya siasa, nimekuja kumuunga mkono Rais
Kikwete katika suala la kupambana na kupinga mauaji ya albino,” alisema Lowasa.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment