HALI ya ulinzi katika viunga vya Jiji la Dar es Salaam
sasa si ya kawaida, kutokana na askari wa Jeshi la Polisi kuonekana kutanda
katika maeneo mbalimbali.
MTANZANIA Jumamosi limebaini jana kuwapo kwa idadi kubwa
ya askari wa Jeshi la Polisi ambao wamesambaa katika maeneo mbalimbali ya jiji,
zaidi wakiwa na silaha kama bunduki na virungu.
Baadhi ya maeneo ambayo gazeti hili limeshuhudia ulinzi
wake kuwa si wa kawaida ni pamoja na Mlimani City, Posta na Namanga.
Pia lilishuhudia magari ya Jeshi hilo (Defender)
yakizunguka na kushusha askari wake katika maeneo hayo ambapo wengine walianza
kusambaa katika mitaa mbalimbali, hususan eneo la Posta Mpya.
Si hivyo tu, katika siku za hivi karibuni eneo la Mlimani
City ulinzi umeonekana kuimarishwa zaidi kuliko ilivyo kawaida.
Kundi la askari limekuwa likionekana karibu na jengo hilo
la Mlimani, hasa karibu na zilipo ofisi za benki ya Twiga Bancorp.
Askari hao pamoja na wengine ambao wamekuwa wakionekana
nje ya lango la kuingilia eneo hilo, baadhi yao wamevalia vifaa ya kuzuia
risasi (bullet proof) na wakati mwingine wakiwa na magari yao.
Katika eneo la Namanga, askari walionekana wakiwa
wamesimama katikati ya makutano ya barabara na wengine wakiwa wamesimama karibu
na miti iliyopo pembezoni mwa barabara hiyo, wakiwa wamebeba silaha zao.
Gazeti hili liliwasiliana na Kamanda wa Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, kuhusiana na hali hiyo ambapo alisema
wapo katika operesheni maalumu ya kupambana na uhalifu ndani ya jiji hilo.
Alisema Jeshi hilo limeamua kuweka askari wake kwa wingi
katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kwa nia ya kuimarisha usalama.
“Kwanza nashukuru ndugu mwandishi kwa kuona jambo hili,
tumelazimika kufanya hivyo kuanzia leo, hii ni kutokana na mahitaji yaliyopo,
tupo makini na imara, tunapambana na uhalifu wa aina zote,” alisema.
Alisema operesheni hiyo imelenga kuimarisha ulinzi katika
maeneo hayo kwa nia ya kupambana na matukio au jaribio lolote la uvunjifu wa
amani ndani ya jiji hilo.
“Hii inaitwa ‘High Police Visibility’, tunajua kwamba
uwepo wa mwonekano wa askari kwa wingi unasaidia kupunguza uwezekano wa kutokea
uhalifu.
“Kazi kubwa tunayofanya ni kudhibiti aina yoyote ya tukio
au jaribio lolote la uvunjifu wa amani na tutawakamata wahalifu wa aina zote
mpaka wapiga debe,” alisema.
Hivi karibuni kundi la kigaidi la Al Shabaab limekuwa
likitoa vitisho kwa nchi zilizoko ukanda wa Afrika Mashariki.
Kundi hilo tayari limefanya mashambulizi nchini Kenya,
ambapo hivi karibuni lilivamia katika Chuo Kikuu cha Garissa, nchini humo na
kuua zaidi ya watu 100.
Hali hiyo imezifanya nchi hizo kuanza kujihami kwa
kuimarisha ulinzi wake katika baadhi ya maeneo yake, hasusan yale yenye
mikusanyiko mikubwa ya watu.
Tanzania ni moja kati ya nchi zilizoko katika ukanda wa
Afrika Mashariki pamoja na Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.
No comments:
Post a Comment