Friday, April 24, 2015

Ujue Ugonjwa wa Macho Mekundu Ambao Unatikisa Dar kwa Sasa

Ugonjwa wa macho mekundu maarufu kama Nairobi Red Eyes umeibuka katika maeneo mbalimbali ya jiji na kuleta usumbufu mkubwa kwa wakazi wengi na kusababisha kushindwa kwa muda kufanya shughuli zao muhimu.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana Ilala, Dk Meshack Shimwela alisema, ugonjwa huo hauna dawa na wengi
wanaougua hupewa tu dawa za kutuliza maumivu.

Alisema ni watu wachache wanaofika katika hospitali hiyo kwa nia ya kupata matibabu, wengi huenda katika hospitali zilizo karibu na maeneo wanayoishi.

“Ugonjwa huu unasababishwa na virusi na hauna dawa. Mtu akija hupewa tu dawa za kutulia maumivu maana wengi huumwa na kichwa,” alisema Dk Shimwela.

Alisema dawa ya kuepuka ugonjwa huo ni kunawa mikono na sabuni kwa kutumia maji ya vuguvugu.

Ugonjwa huo ukoje?

Huu ni ugonjwa unaoshambulia sehemu ya ndani ya jicho iitwayo conjunctiva, sehemu hii ni utando mwembamba wa tishu usio na rangi uliopo ndani ya mfuniko wa jicho ambao inafunika sehemu ya ndani ya jicho iliyo na rangi nyeupe.

Ugonjwa huu huwapata zaidi watoto, unapolipuka husambaa kwa wingi na haraka hasa maeneo ya shuleni, maofisini na majumbani.

Huweza kushambulia macho yote mawili au moja. Ingawa si tishio, mara nyingine huwa na madhara makubwa pale usipotibiwa na kukaa muda mrefu.

Husababishwa na nini?

Ugonjwa huu husababishwa na virusi na bakteria, pia mara nyingine hutokea kwa sababu ya mzio wa macho, vitu kama vumbi, moshi, kemikali au vipodozi.

Red Eyes ya mzio
Hii ni aina ya Red Eyes ambayo imegawanyika sehemu mbili, ipo ambayo huwatokea watu kwa vipindi fulani ndani ya mwaka na nyingine ni ile ya mzio unaosababishwa na kuwapo uchafu nje na ndani ya jicho kwa muda mrefu.

Red Eyes ya uambukizi

Aina hii imegawanyika katika sehemu tatu, ya kwanza inasababishwa na bakteria na hujitokeza mara kwa mara katika jamii.

Mtu huweza kupata aina hii kwa kugusana na mwenye maambukizo.

Aina hii ndiyo inayowapata watu zaidi kuliko nyingine, huenezwa na virusi vinavyosababisha mafua, majimaji ya kikohozi na chafya. Ndiyo ya hatari zaidi na ina madhara makubwa kama isipotibiwa mapema.

Red Eyes ya kemikali

Hii husababishwa na kemikali zinazokereketa hasa maeneo yenye uchafuzi wa hali ya hewa kama vile miji yenye viwanda vingi na kemikali zinazowekwa katika mabwawa ya kuogelea.

Dalili za ugonjwa

Huweza kuwa katika jicho moja au mawili, kujihisi macho kama yana mchanga, macho kuuma, kuwasha na kutoa machozi mara kwa mara.

Nyingine ni macho kutoa uchafu, kuwa mekundu au rangi ya pinki, kuvimba, kukosa uvumilivu wa mwanga na kupata homa ya kiwango cha chini.

Uchunguzi na tiba

Uchunguzi hufanyika katika kliniki maalumu za macho zenye wataalamu, kwa wale waliopata uambukizi hutibiwa na antibaotiki za kuweka katika macho.

Wenye mzio hupewa dawa za kutuliza na kuzuia na wenye uambukizi wa virusi hakuna tiba maalumu zaidi ya kinga ya mwili kutatua tatizo hilo.
Kama chanzo ni kemikali huweza kutumia maji yenye chumvi kama saline, kuoshea machoni pamoja na dawa za kupunguza mzio na maumivu.

Namna ya kujikinga

Usafi wa kimwili kwa ujumla ni muhimu kwani unapunguza kuenea kwa ugonjwa huu. Acha kukimbilia miwani unapopata ugonjwa huu na fika katika huduma za afya haraka pale unapoona dalili.

Ufanye nini unapougua

1. Acha kutumia mikono kushika macho yako

2. Osha mikono yako kila mara

3. Osha au fua taulo au kitambaa unachotumia na pia usishirikiane na mtu mwingine vifaa hivyo.

4. Acha kutumia vipodozi hatari.

Nyongeza na Dk Shita Samwel

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment