Serikali imeanza kutimiza ahadi yake ya kuyafuta
mashirika na asasi zisizo za kiserikali, NGO, yakiwamo ya kidini na kwa kuanzia
imetangaza kusudio la kuzifuta asasi 24 katika kipindi cha siku saba kuanzia
jana.
Miongoni mwa asasi hizo ni
taasisi mbili za dini ambazo
ni Tanzania Muslim Social Community na Tanzania Christian Outreach Ministries
ambazo zimepewa siku saba kujitetea.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Issack Nantanga
aliliambia MWANANCHI kuwa asasi zote zitakazothibitika kwenda kinyume na
malengo ya kuanzishwa kwake, zitafutwa.
Nantanga pia alisema panga hilo litazipitia pia asasi
ambazo zimekuwa haziwasilishi kwa msajili ada ya kila mwaka na taarifa za fedha
zilizokaguliwa na wakaguzi waliosajiliwa.
“Haya mashirika 24 ndio tumeanza nayo na ukaguzi
unaendelea. Tumetoa muda wa siku saba kuanzia leo (jana) kujitetea kwanini
yasifutwe na wakishindwa kufanya hivyo, yatafutwa rasmi,” alisema.
Aliyataja mashirika mengine kuwa ni Kagwa Development
Society, Morning Star Production Training Centre, Chama cha Kujitegemea na Kujiendeleza
na The Organisation of Tanzania Community.
Mashirika mengine ni Mbezi Juu and Salasala Woman
Agricultural and Environmen Association, Waridi Training Society, Vituka
Machimbo Development Association na Gerezani Nguvukazi.
Mengine ni Nyakasangwe Small Scale Farmers Association,
Vitendo Trust Fund, Bahari Beach Silvers and Woman Association, Owners Social
Club na Magovent Development Association.
Kwa mujibu wa Nantanga, mashirika mengine yaliyomo katika
orodha hiyo ni Hananasifu Quarters Women Association, Mburahati Barafu
Development Community na The Movers Club.
Pia yamo Umoja wa Maendeleo ya Jamii Mlima Mindu, Tabata
Tujiimarishe Club, Umoja wa Wauza Miche Ubungo, Kunguru/Kinzudi Development
Association na Women & Environment Association.
“Ukitazama katika tovuti ya wizara utakuta tuna orodha ya
mashirika 10,624 yaliyosajiliwa tangu 1953. Tutapitia moja baada ya jingine na
yatakayobainika kukiuka sheria yatafutwa,” alisisitiza.
Wakati Serikali ikianza mchakato huo, imebainika kuwa
baadhi ya klabu za waandishi wa habari za mikoa, nazo ziko hatarini kuangukiwa
na rungu hilo kwa kutolipa ada. Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi
ya klabu hizo za waandishi wa habari hazina taarifa za fedha zilizokaguliwa na
wakaguzi waliosajiliwa na wala taarifa hizo haziwasilishwi kwa msajili.
Hatua hiyo ya Serikali kuanza kuyafuta mashirika hayo
imekuja takribani wiki mbili baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias
Chikawe kutangaza mpango wa kuyafuta mashirika yanayokiuka sheria.
Uamuzi huo wa Serikali ulitangazwa siku chache baada ya taasisi
za dini nchini kutoa matamko mbalimbali kluhusu mchakato wa kuandika Katiba
mpya, likiwamo Jukwaa la Wakristo ambalo liliwataka waumini kuikataa Katiba
Inayopendekezwa kwa kuipigia kura ya hapana.
Jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT), Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) na Umoja wa Kanisa
la Pentekoste Tanzania (CPCT).
Jukwa hilo linadai kuwa Serikali imewaahidi Waislamu
kuingiza Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba ili waipigie kura ya ndio Katiba
Inayopendekezwa, jambo ambalo limesema linaweza kusababisha mgawanyiko.
Tamko hilo lilijibiwa na taasisi za Kiislamu zilizosema kuwa
suala la Mahakama ya Kadhi ni haki yao na kuwataka viongozi hao wa Kikristo
kuwaacha waumini wake wajiamulie wenyewe mambo ya Katiba.
Katika tamko lake, Chikawe alizionya taasisi hizo za
kidini dhidi ya kujihusisha na shughuli zilizo kinyume na malengo ya kuanzishwa
kwake, akitaja kitendo cha kuwataka waumini wapige kura ya kuikataa Katiba
Inayopendekezwa.
Pia zilitishia kutoikubali Katiba Inayopendekezwa iwapo
Serikali haitatekeleza ahadi yake ya kuingiza suala hilo kwenye Katiba.
Chikawe alisema kuanzia Aprili 20, Serikali ingezifuta
taasisi zote zilizosajiliwa chini ya wizara yake ambazo haziwasilishi taarifa
zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada za kisheria.
Chikawe alisema Serikali inatoa onyo kwa taasisi za dini
ambazo zimetoa matamko ya aina hiyo kwamba wasirudie tena vinginevyo Serikali
itakuwa haina njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuyafuta.
Alisema waumini wana haki ya kuamini mafundisho ya dini
zao, lakini wanapaswa kutekeleza masuala yao ya kisiasa na kijamii kwa utashi
wao bila ya kushawishiwa na mtu yeyote kama sheria zinavyotaka.
“Mfano ni pale viongozi wa dini wanapochangisha fedha za
kuandamana au kukutana na wanasiasa na kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali
za uongozi,” alisema Chikawe.
“Hii si kazi ya taasisi za dini na ni kinyume na sheria,”
Hata hivyo uamuzi huo wa Serikali ulipokelewa kwa hisia
tofauti na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa Dini, wakisema uamuzi huo una
lengo la kuwafunga midomo wasikemee maovu.
Viongozi wa dini walienda mbali na kudai wamesema taasisi
zao zinawakilisha watu hivyo zina haki ya kikatiba na kisheria kupinga jambo
lolote zitakaloona linakwenda kinyume na maslahi ya Taifa.
No comments:
Post a Comment