MFANYABIASHARA Farijala Hussein aliyemaliza kifungo kwa
kuiba fedha za akaunti ya EPA, amehukumiwa tena kwenda jela baada ya kupatikana
na hatia katika kesi nyingine ya wizi wa zaidi ya Sh milioni 400 katika akaunti
hiyo.
Vilio vilitawala katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu
jijini Dar es Salaam baada ya Farijala kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu kwa
kila kosa na kurudisha zaidi ya Sh milioni 400. Mahakama ilimpa adhabu Farijala
ya kwenda jela jumla ya miaka 15 kwa makosa matano aliyotiwa hatiani.
Farijala na mwenzake aliyeachiwa huru, Ajay Somani
walisomewa hukumu jana na jopo la mahakimu linaloongozwa na Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu, Projestus Kahyoza.
Farijala aliwahi kuhukumiwa katika mahakama hiyo na
kutiwa hatiani katika kesi namba 1161 ya mwaka 2008 na kesi namba 1164 ya mwaka
huo kwa mashtaka kama hayo ya kughushi na kujipatia fedha kwa udanganyifu
katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jopo lilisema kwamba washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na
mashtaka sita yakiwamo ya kula njama, kughushi nyaraka mbalimbali na kujipatia
Sh 455,874,624.51 kwa kutumia nyaraka za uongo kutoka BoT, fedha ambazo
zilikuwa katika akaunti ya madeni ya nje (EPA).
Hakimu Francis Kabwe alisema Ajay anashtakiwa kwa makosa
mawili; kula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wakati Farijala
anashtakiwa kwa mashtaka sita yakiwamo kula njama, kughushi na kujipatia fedha
kwa njia ya ufanganyifu.
“Katika shtaka la kwanza upande wa mashtaka umeshindwa
kuthibitisha kwamba washtakiwa walikula njama kutenda kosa la kujipatia fedha,
hivyo mahakama inawaachia huru washtakiwa wote,” alisema.
Katika shtaka la pili la kughushi, hakimu alisema hati ya
usajili wa Kampuni ya Ruaha Investment upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha
kwamba mshtakiwa Farijala alighushi, hivyo inamtia hatiani.
Pia mahakama hiyo ilimtia hatiani Farijala baada ya
kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba aliwasilisha nyaraka hiyo ya
kughushi benki, alighushi hati ya makubaliano wakionyesha kwamba wanapaswa
kuhamishiwa zaidi ya Sh milioni 400 na kuiwasilisha benki na mshtakiwa huyo
ndiye aliyejipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu.
“Mshtakiwa wa pili Ajay hakula njama kutenda kosa,
mshtakiwa wa kwanza Farijala tu ndiye aliyeghushi na kuwasilisha nyaraka
zilizoghushiwa kwa nia ya kujipatia fedha, hivyo mashtaka dhidi ya mshtakiwa wa
pili hayajathibitishwa.
“Jamhuri pamoja na kuwasilisha mashahidi saba mahakamani,
walishindwa kuthibitisha bila kuacha shaka shtaka la kula njama na shtaka la
kujipatia fedha lililokuwa linamkabili mshtakiwa wa pili,” alisema hakimu Kabwe.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment