HATIMAYE Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewatoa hofu Watanzania kuhusu afya
yake kwa kueleza kuwa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa uchunguzi wa
matatizo yake ya uti wa mgongo.
Kardinali Pengo pia amegusia nafasi ya urais katika
Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwataka watanzania kumchagua rais fukara kuliko
anayetafuta nafasi hiyo kwa rushwa.
Alitoa kauli hiyo
katika mahafali ya Saba ya Chuo Kikuu
cha Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam jana.
Alisema maradhi ya uti wa mgongo ambayo yamekuwa
yakimsumbua kila yaligundulika Agosti mwaka 2013 baada ya kufanyiwa uchunguzi
wa afya, Ujerumani.
“Hospitali ya Ujerumani ndiyo waligundua kuwa nyuzi mbili
ndani ya uti wa mgongo zimechanika zinabana mashipa ya neva, kwa hiyo zikawa
zinanisababishia maumivu ya mgongo.
“Kule Ujerumani walizirudisha katika nafasi yake lakini
kwa bahati mbaya hawakufunga huku wakitegemea kuwa mambo yatakwenda vizuri kwa
njia ya kawaida.
“Lakini kwa sababu ya kurukaruka nikajiona kama nimepona
ila baada ya muda kidogo maumivu yasio ya kawaida yalirudi tena,” alisema
kiongozi huyo wa kiroho.
Alisema maumivu yalipozidi Juni mwaka jana alisafiri
kwenda Hospitali ya Manipal, Bangalore, India kwa uchunguzi zaidi.
“Walinihudumia vizuri na kwa sasa naendelea vizuri … kwa
wale wanaojali uhai wangu nilipokwenda mara ya mwisho kwenye uchunguzi
waliniambia kila kitu kimekaa kwenye nafasi yake.
“Madaktari walinielezea kuwa nisishangae maumivu ya mara
kwa mara kwa sababu operesheni ilikuwa kubwa.
“Kwa sababu operesheni ya sasa itachukua muda kati ya
miaka miwili hadi mitatu niweze kujisikia mzima kabisa. Kwa sasa naendelea
vizuri sina tatizo zaidi,” alisema.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka
huu, Kardinali Pengo alisema ni kitu kibaya kama viongozi wanaowania nafasi ya
urais wanatoa rushwa.
“Uongozi wa Taifa hauwezi kununuliwa kwa gharama yoyote…
wanaoelekea kutoa rushwa baadaye watataka sisi wananchi tulipe zile gharama
ambazo walikuwa wametugawia katika kutoa rushwa, afadhali waache kabisa.
“Ni vizuri tupate rais anayekuwa fukara lakini anayependa
nchi yetu na hatatudai gharama ya kumchangua kama si hivyo gharama inaweza kuwa
kubwa ikatusababishia matatizo,” alisema.
Kardinali Pengo pia alizungumzia matukio ya ugaidi na
kuwataka wanaosambaza ujumbe fupi wa vitisho kuacha mara moja tabia hiyo kwa
vile inawaweka wananchi katika hofu.
“Wanaweza kusababisha taharuki na mikanganyiko na kuleta
madhara kwa wengi kwa kitu ambacho hakipo.
“Kama kuna hofu ya usalama sehemu yoyote inabidi
tuwaachie wataalamu wa usalama waweze kuishughulikia kwa namna wajuavyo,”
alisema.
Hata hivyo, aliitaka serikali kupitia Idara ya Usalama
kuwa ya kwanza kuwahakikishia wananchi kuwa hakuna matukio hayo amani na
utulivu viendelee kuwapo.
Pia aliwashauri wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Josesph kuwa wasisome kwa ajili ya kuajiriwa na serikali tu.
“Kuna nafasi za wataalamu wa sayasi na sanaa za kujiajiri
katika chuo hiki … Chuo kikuu kizuri ni kile kinachoandaa wanafunzi kujiajiri,”
alisema.
Mkuu wa Chuo hicho, Padre Aru Raji alisema chuo kinazidi
kupanuka na mwaka huu kinatarajia kufungua Chuo Kikuu Sumbawanga na Chuo cha
Afya na Tiba, Boko, Dar es Salaam.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment