Ikulu imekana kuwapo njama zozote za kutaka kumuangamiza
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, zilizodaiwa kuandaliwa na Rais
Jakaya Kikwete, kwa kile kilichodaiwa kuwashughulikia wanaoihujumu serikali
yake na kupanga kumshughulikia.
Njama hizo ziliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari,
ambavyo vilidai
kunasa mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Kiongozi wa chama cha
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye anadaiwa kumchongea Dk. Mengi kwamba, ndiye
kinara anayesababisha serikali yake iyumbe kila mara.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory
Rweyemamu, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais Kikwete hawezi
kushiriki katika njama za kumdhuru raia na kwa hiyo, habari hizo ni za
kutengenezwa kwa nia mbaya ya kutaka kuharibu urafiki uliopo kati ya Rais na
Dk. Mengi.
Alisema Rais Kikwete alizisikia habari hizo akiwa nchini
Jordan, Jumamosi ya wiki iliyopita na kushangazwa nazo.
Hata hivyo, alisema Zitto, ambaye ndiye wa kwanza
kushutumiwa kuhusiana na habari hizo alikwishazijibu kwa kuzikanusha na kwamba,
juzi Dk. Mengi alihudhuria sherehe za kutunuku nishani Ikulu, hivyo haamini
kwamba, mahali pabaya kiasi hicho, ambako kuna watu wanamsubiri ili kumdhuru,
anaweza kwenda.
Alisema madai kwamba, Zitto na Rais Kikwete walikutana
Ikulu na kuzungumzia suala hilo, hayana ukweli, kwani hakuna mkutano wa ana kwa
ana au mazungumzo ya simu, yaliyofanyika kati ya viongozi hao wawili katika
miezi ya hivi karibuni.
“Hata wakati huo, ambao ingetegemewa wangewasiliana labda
kwa namna ya mazingira ya wakati huo wa matatizo ya Escrow na nini na nini,
hawakuwasiliana kwa sababu Rais alikuwa anatibiwa nje ya nchi. Kwa hiyo,
hapakuwapo na mkutano wa namna hiyo wa mbinu sijui za kupanga mbinu za
kumuumiza mtu,” alisema Rweyemamu.
Alisema pia Rais huapa kulinda raia wote na mali zao,
hivyo hawezi kugeuka na kuanza kula njama za kujaribu kumdhuru raia yeyote
nchini.
Rweyemamu alisema pia Rais Kikwete na Dk. Mengi
huwasiliana sana, kwani anayo simu yake na amekuwa akimpigia mara nyingi na
kuzungumza naye, hivyo alidhani busara bora zaidi kwenye jambo hilo, ingeongoza
kwamba, Dk. Mengi angempigia Rais na kutaka kujua ukweli kuhusiana na habari
hizo.
“Wakazungumza wote wawili, watu wazima, wazee wenye
busara sana wakaelewana, kwamba tumeliruhusu hili suala kutoka pale
lilipotakiwa kuja, tukalitumbukiza kwenye ukumbi wa kila mtu wa hadhara inakuwa
jambo gumu kidogo kueleweka,” alisema Rweyemamu.
Aliongeza: “Ndio maana nikasema tulipopata habari, sisi
hatukujua tu-react (tujibu) vipi. Yaani kwa sababu jambo halipo, jambo
limetungwa, limefinyangwa finyangwa hivi likatupwa hivi mbele ya watu, hatujui
limeanzia wapi. Hata unapoiambia Ikulu, Kurugenzi ya Mawasiliano sijui,
Mkurugenzi wa (Idara ya) Habari (Maelezo) hawakujibu. Tujibu nini? Hatujui. Kwa
hiyo ndio maana sasa tukaanza sasa kuwasiliana jamani kuna hili tufanye nini?
Tena kuna watu wengine walikuwa wanasema bwana hata ukiulizwa usiliseme. Kwamba,
ni jambo halipo, halina maana, tuachane nalo lipite.”
Hata hivyo, alisema jana alilazimika kulizungumzia kwa
kuwa aliulizwa na waandishi wa habari, pia kwa vile anayeshutumiwa ni Rais na
shutuma zinahusu usalama wa raia wake, hivyo alifanya hivyo ili wananchi wapate
kupumua japo kidogo.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment