ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima,amesema haogopi mtu yeyote wala kufa bali ataendelea kuinyoosha nchi
anapoona haiendi sawa.
Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana,wakati wa mahubiri
yaliyofanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers Kawe.
Kwa mujibu Askofu Gwajima, baadhi ya watu wamekuwa
wakimhusisha kuwa na urafiki na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa jambo
ambalo alikiri ni la ukweli kwa sababu walifahamiana tangu mwaka 1996.
“Niliwahi kumuita Waziri Mkuu Mizengo Pinda mara nne hapa
ili aje azindue moja ya kazi zangu,hakuja badala yake nilimuita Lowassa na
aliitikia wito wangu na kuja kuifanya kazi hiyo hivyo siwezi kumuacha.
“Wapo viongozi wengi ambao wanakuja kusali katika kanisa
langu, kwa mfano Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Nape Nnauye, kwa nini
wasimseme yeye badala yake wanamsema Lowasa tu?.
“Nashangaa mnatoka mlipotoka mnaongea kwa kubana pua,
ukimuogopa mtu nchi itakuwa haiendi vizuri na mimi sitaogopa kukemea mambo
ambayo hayafai katika jamii, mfano suala la Escrow.
“Nitaendelea kuinyoosha nchi ninapoona haiendi sawa.
“Siwezi kwenda mbali na Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk.Willbrod Slaa hata kama atakuwa Rais… na yeye pia ni rafiki yangu,” alisema
Askofu Gwajima.
Katika ibada hiyo aliliombea Taifa amani, uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na kikao kijacho cha Bunge la Bajeti
linalotarajia kuanzia baadaye mwezi ujao.
Wiki iliyopita, Askofu Gwajima alifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mashitaka mawili ambayo ni kumtolea lugha
ya matusi ambayo imemfedhehesha Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar
es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, na kuweka vibaya silaha
anayomiliki.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment