MAHOJIANO baina ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima na Jeshi la Polisi yaliyokwama wiki iliyopita kutokana
na kuzorota kwa afya ya askofu huyo, yaliendelea jana saa sita huku akitakiwa
kuwasilisha nyaraka muhimu kumi siku ya mahojiano mengine yatakayofanyika wiki
ijayo.
Hali hiyo imeonekana kumchanganya wakili wa
kiongozi huyo wa kiroho,
kiasi cha kusema hakutegemea kama ingefikia hatua hiyo, kwani alitarajia mteja wake angehojiwa juu ya matumizi ya lugha ya matusi dhidi ya kiongozi mwingine wa dini nchini.
kiasi cha kusema hakutegemea kama ingefikia hatua hiyo, kwani alitarajia mteja wake angehojiwa juu ya matumizi ya lugha ya matusi dhidi ya kiongozi mwingine wa dini nchini.
Akizungumza mara baada ya mahojiano hayo katika
Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, Gwajima aliyeonekana kuwa na afya njema
tofauti na wiki iliyopita alipowasili Polisi na kushindwa kupanda ngazi kiasi
cha kusababisha kuahirishwa kwa mahojiano, alisema mahojiano ya jana
yalifanyika vizuri na yanatarajiwa kuendelea Aprili 16 mwezi huu na kutakiwa
kupeleka nyaraka muhimu kwa mahojiano zaidi.
Akielezea jinsi mahojiano yalivyokuwa, Wakili
anayesimamia kesi hiyo, John Mallya alisema
mahojiano yamekwenda vizuri, lakini
amesikitishwa na mambo ambayo mteja wake ameulizwa kwani walidhani wataulizwa
kuhusiana na matumizi ya lugha chafu ambayo polisi walidai mchungaji aliitumia
kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini.
“Mahojiano yamekwenda vizuri lakini nasikitika
sana kutokana na mambo waliyokuwa wanamhoji. Wamemuuliza mambo ambayo
hayahusiani kabisa na kile tulichotarajia na ndicho kilichotuleta hapa,
nilidhani mteja wangu ataulizwa kuhusiana na matumizi ya lugha chafu iliyodaiwa
kutumika kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini,” alihoji wakili wa
Gwajima.
Aliendelea kusema kuwa, mambo aliyoulizwa ni
kuhusiana na ukoo wake, wazazi wake hata ndugu zake na watu wengine wa kwao
waliokufa.
Alisema walihoji pia juu ya mambo mengine kama
umiliki wa helikopta, utajiri wake, nyumba anayoishi, uhusiano wake na watu
mbalimbali.
“Nimeshangaa sana kuona mteja wangu ameulizwa
vitu kama hivyo ambavyo havihusiani na madai ya hapo awali ya matumizi ya lugha
ya matusi.
Tumeagizwa tulete nyaraka kumi siku ya mahojiano yetu tena
yatakayofanyika tarehe 16 mwezi huu na sisi tutafanya hivyo,” alisema
Mallya.
Alizitaja nyaraka na vitu vingine wanavyotakiwa
kuvipeleka Aprili 16 ni hati ya usajili wa kanisa, bodi ya udhamini wa kanisa
na majina yao, idadi ya makanisa yaliyopo chini yake, na muundo wa uongozi wa
kanisa lake.
Vingine ni namba ya usajili wa kanisa, ritani za
kanisa lake (mapato na matumizi ya fedha za kanisa lake), mtu anayechukua na
kurekodi mkanda wa video kanisani kwake, pamoja na waraka wa Baraza la Maaskofu
uliosomwa makanisani.
Hata hivyo mapema jana asubuhi wafuasi wake
walifika kwa wingi kituoni hapo huku wengine wakiwa wamevalia sare za Kikosi
cha Polisi Jamii na wengine wakiwa wamevaa mavazi yanayovaliwa na viongozi wa
dini yenye kola nyeupe kuonesha kuwa wao ni viongozi wa kanisa hilo.
Hali ya usalama ilikuwa imeimarishwa vya kutosha
katika kituo hicho cha Polisi huku askari wa Kikosi cha Polisi Jamii kutoka
katika kanisa la Gwajima wakiwa wamejipanga kuanzia lango la kuingilia kituoni
hapo na kuachia hatua kadhaa mithili ya kumsubiri na kumpokea mfalme.
Hali hiyo iliwashangaza wakazi wengi wa jiji la
Dar es Salaam waliokuwa wanapita karibu na eneo la kituo kikuu cha Polisi, na
kusababisha hata wengine kuhatarisha usalama wao kutokana na hatari ya kugongwa
na magari pamoja na vyombo vingine vya moto.
Mara baada ya kutoka kuhojiwa, wafuasi wake
walishangilia na kurukaruka huku wakitanda barabara ya Stesheni na kusababisha
adha ya usafiri kwani ilikuwa ni vigumu kwa magari kupita kutokana na
purukushani na shangwe za wafuasi wa kiongozi huyo wa kiroho waliokuwa
wametanda barabarani.
Hata hivyo, uwepo wa wafuasi hao ulikuwa ni
kinyume cha sheria kwani tayari polisi walishapiga marufuku wafuasi hao kufika
kituoni hapo wakati kiongozi wao akihojiwa.
Gwajima aliingia matatani mwishoni mwa mwezi
uliopita na kujikuta akitakiwa kujisalimisha Polisi baada ya kutakiwa kufanya
hivyo kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya kumkashifu Askofu Mkuu wa
Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo.
Katika siku ya kwanza aliyojisalimisha, Gwajima
aliripotiwa kuzimia wakati akihojiwa na makachero wa Polisi kuhusiana na tuhuma
dhidi ya Askofu Pengo, hali iliyosababisha akimbizwe hospitali ya TMJ,
Mikocheni kwa matibabu alikokuwa kwa siku nne kabla ya kuachiwa kwa dhamana
wakati akisubiri mahojiano zaidi.
Akiwa hospitalini hapo, wafuasi wake 15 wakiwemo
wachungaji sita, mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na
mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Matibabu na
Teknolojia (IMTU), Dar es Salaam walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za
kutaka kumtorosha askofu huyo kutoka hospitalini.
Ilielezwa kuwa, baada ya kuwapekua, watu hao
walikutwa na begi lenye bastola aina ya BERRETA yenye namba CAT5802 ikiwa na
risasi tatu, risasi 17 za Short gun na vitabu viwili vya hundi.
Begi hilo liliripotiwa kuwa na hati ya kusafiria
yenye jina la Gwajima Joseph Mathias yenye namba AB 544809, kitabu cha hundi
cha Benki ya Equity, nyaraka mbalimbali za kampuni ya PUMA, chaja ya Simu na
Tablets, suti mbili na nguo za ndani.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment