Watu watano wamejeruhiwa katika tukio linalodaiwa kuwa la
kigaidi baada ya kulipuliwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu. Tukio hilo
inasemekana kutokea siku ya maadhimisho ya Mei mosi, katika kijiji cha Msolwa
ujamaa, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Aidha, tukio hilo limetokea karibu na eneo ambalo siku
chache zilizopita, jeshi la polisi lilikamata watu 10
wakiwa na milipuko 30,
sare za jeshi, majambia, risasi, bendera, vitabu na madaftari wakiwa ndani ya
msikiti katika kijiji cha Kidatu wilayani hapa.
Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, saa 2.00 usiku juzi katika kijiji cha Sanje.
Alisema wananchi wa eneo hilo waliwaona vijana wawili
wakipita katika eneo hilo na kuwatilia mashaka kutokana na muonekana wao.
Alisema mpaka sasa hajapata taarifa kamili za chanzo cha
tukio, lakini alisema inawezekana ni muendelezo wa matukio ya kihalifu
yaliyotokana na kukamatwa kwa watuhumiwa 12, waliokutwa na vitu mbalimbali
ikiwamo milipuko hivi karibuni.
Alisema katika tukio hilo, watu watano wamejeruhiwa
akiwamo dereva wa gari la halmashauri linalotumiwa na mwenyekiti wake, David
Ligazio, ambalo limevunjwa kioo cha nyuma na mbele kikipasuliwa na mlipuko huo.
Alisema majeruhi wote akiwamo dereva wa gari hilo lenye
namba za usajili SM 10632, Novatus Ngope (47), walikimbizwa katika kituo cha
afya cha Nyandeo na baadaye kuhamishiwa
Hospitali ya Mtakatifu Kizito, wilayani Kilosa.
Katika tukio hilo, Ligazio akiwa mgeni rasmi katika
maadhimisho ya sikukuu hiyo kata ya Sanje, alikuja Mwenyekiti wa kitongoji
hicho Joseph Mhenga akiwa na vijana wawili walioonekana si wenyeji wa eneo
hilo.
Alisema mwenyekiti huyo alitaka ushauri kuhusu vijana hao na ndipo alipoamuru
wapelekwe katika kituo cha polisi.
Alisema kabla ya kupelekwa kituoni, vijana hao
walipekuliwa na mmoja wa askari mgambo na kukutwa na bomu ambalo walilitoa
na kulirushia kwenye gari la mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero.
Alisema bomu hilo lililipuka na kumjeruhi dereva na watu
wengine wanne akiwamo askari mgambo ambayo hali yake ni mbaya.
Aliwataja wengine kuwa ni Amos Msopole(29) na Azama
Naniyunya (59), ambao wamelazwa
hospitali ya Mt. Kizito, Mikumi wilayani Kilosa.
Akizungumzia tukio hilo, Afisa Mtendaji wa kata ya Sanje,
Hawa Ndachuwa, alisema siku ya tukio watu wawili walikodi pikipiki kutoka
Kidatu na kuomba wapelekwe Mkula.
Hata hivyo, dereva wa bodaboda aliwatilia shaka na
kujifanya anawaomba wamuongezee fedha za malipo kwani mapatano hayakulingana na
umbali.
Alisema watu hao walikubali kumuongezea fedha na
walimwomba kuwaonyesha sehemu ya kutolea fedha. Wakati wakihangaika kutoa
fedha, mwendesha bodaboda huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji.
Alisema baada ya wananchi kuwaona watu hao, walipatwa na
mshituko kutokana na mavazi yao na kuanza kuwapekua chini ya ulinzi wa askari
mgambo wa kijiji.
Alisema mtuhumiwa mmoja alikutwa na viberiti vya gesi na
mwingine alikuwa mgumu kutoa ushirikiano na wananchi walizidi kumtilia shaka
baada ya kuona kuwa ana kitu alichokihifadhi katika kiuno.
Alisema wakati wanaendelea kuwapekua mtuhumiwa wa kwanza
alifanikiwa kukimbia. Aidha, wakati wanajiandaa kumdhibiti wa pili alitoa kitu
kinachofanana na bomu na kurusha lilipo hilo gari la mwenyekiti na kutoa
mlipuko mkubwa na yeye kufanikiwa kukimbia.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonald Paul,
alipotafutwa kwa njia ya simu, msaidizi wake alisema amekwenda eneo la tukio.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito,
Maximilian Mwenda, alithibisha kupokea majeruhi wanne.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment