Sunday, May 3, 2015

Mnaofanya biashara zenu chini ya njia kubwa za kusafirishia umeme mko hatarini kupungukiwa na nguvu za kiume.....Au kama ni mjamzito kuharibu mimba....Ni kutokana na mionzi

WAFANYABIASHARA wadogo na waendesha bodaboda wanaofanya biashara zao kwenye njia kubwa za kusafirishia umeme wapo hatarini kupungukiwa nguvu za kiume.

Kutokana na kuwepo wengi kwenye njia hizo kubwa za kusafirishia umeme,
wametahadharishwa kutoendelea kufanya biashara kwenye maeneo hayo.

Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Mahusiano Msaidizi huduma kwa wateja wa Tanesco Mwanza, Haji Bwegege wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa maonyesho ya siku ya wafanyakazi uliofanywa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kwenye viwanja vya Furahisha, jijini hapa.

“Tumekuwa tukiielimisha jamii mara kwa mara kutofanya biashara kwenye njia ya umeme mkubwa unaopita kutokana na madhara wanayoweza kuyapata na hii ya kupungukiwa nguvu za kiume ni moja ya madhara ambayo yanaweza kuwapata hivyo wachukue tahadhari mapema,” alisema.

Aliyataja madhara mengine kuwa pamoja na mwili kupoteza nguvu kutokana na mionzi hivyo wananchi kutakiwa kuishi umbali wa mita 30 kila upande pamoja na mjamzito kuharibu mimba.

Akizungumzia suala la ‘Vishoka’, Bwegege aliwataka wananchi wasikubali kuuziwa fomu majumbani kwani fomu za kuomba kuunganishiwa umeme hutolewa ofisini tu ama pale maofisa wao wanapotembelea vijijini wakiwa na vitambulisho na kutoa risiti.

“Mnatambua kuwa miradi ya umeme vijijini inaendelea ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Electricity five (F5) hivyo vishoka kutumia nafasi hiyo kuwarubuni wananchi ambapo wamekuwa wakifika vijijini na kuwauzia fomu kati ya Sh 60,000 na 100,000 wakati bei halisi ya fomu ni Sh 5,900 tu,”alisema.

Alisema vishoka hao wamekuwa wakijitokeza katika maeneo ya vijijini ambapo miradi hiyo imekuwa ikiendelea na kwamba kama Tanesco wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kufanya mikutano ya hadhara na kuwataka wananchi wajiandikishe kwenye ofisi za serikali za vijiji.

Bwegege alisema chini ya miradi ya wakala wa umeme vijijini, wananchi wanaozungukwa na mradi hutozwa Sh 27,000 kama gharama ya kuungiwa umeme.

Alisema wameshiriki katika maonesho hayo ili kutoa elimu kwa jamii juu ya shughuli zao na kwamba huduma zote zinazotolewa ofisini zinatolewa uwanjani hapo.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment