Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt.
Agnes Kijazi anasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu mstaafu
Dkt. Mohamed Mhita (pichani) aliyezaliwa tarehe 17 Februari 1946 na kufariki
siku ya Jumatatu tarehe 06 Aprili 2015
katika hospitali ya Agakhan jijini Dar
es Salaam.
Dr. Mhita kwa kushirikiana na uongozi wa iliyokuwa idara Kuu ya Hali
ya Hewa alishiriki katika kuishauri Serikali kuhusu kuanzishwa kwa Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania kutoka iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa.
Pamoja na nafasi ya Mkurugenzi Mkuu pia alikuwa
Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani kuanzia
mwaka 1992 hadi 2008. Alichaguliwa kuwa Mjumbe katika Baraza Kuu la Shirika la
Hali ya Hewa Dunia kuanzia mwaka 1995 hadi 2007.
Alichaguliwa kushika nafasi ya Rais wa Jumuiya ya Hali ya
Hewa katika Bara la Afrika (RA 1)
kuanzia mwaka 1998 hadi 2007. Dkt Mhita alikuwa Rais wa ‘Tanzania
Meteorological Society’ sambamba na nafasi nyingine nyingi mbalimbali
alizoshika ndani na nje ya nchi.
Akielezea baadhi ya mambo makubwa yatakayomfanya Dkt.
Mhita aendelee kukumbukwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini
Dkt. Agnes Kijazi alisema ‘Dkt. Mhita atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa
katika kuendeleza sayansi ya hali ya hewa hapa nchini, katika Bara la Afrika na
Duniani kwa ujumla hususani katika ushiriki wake wa kuianzisha Mamlaka ya Hali
ya Hewa nchini kwa kuandaa dira (vision) na dhamira (mission) ya Mamlaka kwa
kipindi cha miaka kumi na tano (15) kuanzia mwaka 2000 hadi 2015’.
Dkt. Mohamed Mhita ni mmoja kati ya wanasayansi waliokuwa
zao la chuo kikuu cha Stolkholm, Sweden ambako alitunukiwa shahada ya hali ya
hewa (BSc. Met) mwaka 1977. Kuanzia
mwaka 1981 hadi 1984 alikuwa mafunzoni katika
chuo Kikuu cha Reading, Uingereza ambako alitunikiwa shahada ya uzamivu
(PhD). Hapa nchini alipata mafunzo ya Sekondari katika shule za Tanga na
Karimjee zote zikiwa mkoani Tanga.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inajumuika na familia,
ndugu, jamaa na marafiki katika kuomboleza msiba huu.
Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa Jina lake lihimidiwe.
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI AFISA MAHUSIANO MAMLAKA YA
HALI YA HEWA TANZANIA.
No comments:
Post a Comment