Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba |
WANAWAKE wenye umri mkubwa wametakiwa kuacha
kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na vijana wenye umri mdogo, kwani jambo
hilo linawapunguzia heshima katika jamii.
Ushauri huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya
Kibaha, Halima Kihemba wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani
yaliyofanyika eneo la Kituo cha Afya Mlandizi, wilayani Kibaha mkoani
Pwani.
Kihemba, ambaye kitaaluma ni mwanahabari,
alisema kuna ripoti za kipolisi mkoani Pwani zinazoeleza kuna kinamama ambao
tayari wamevuka umri wa miaka 60 wana uhusiano wa kingono na vijana wenye umri
mdogo, jambo linalowapunguzia heshima katika jamii.
“Kuna taarifa kuwa miongoni mwenu kuna kina mama
wana tabia mbaya ya kuwa na wapenzi ambao ni vijana wadogo sana kiumri. Kweli
si kweli? Aliuliza mkuu huyo wa wilaya na wazee hao ambao kwa idadi walikaribia
300, wakaitikia ‘Kweliiiii’.
Baadaye, HabariLeo lilimfuata Kihemba na
kumwuliza juu ya ukubwa wa tatizo hilo mkoani humo ambapo alijibu; “Halijawa
tatizo kubwa sana, lakini kuna wachache walio na tabia hizo mbaya, ndio maana
tunaanza kulidhibiti ili lisisambae kwa kasi maeneo mengine.”
Alisema tatizo hilo kwa ukubwa lipo miongoni mwa
wanaume ambao wamekuwa wakijihusisha na ndoa za utotoni kwa muda mrefu, huku
likilazimisha wanafunzi wa kike kukatisha masomo yao kuolewa.
Uchunguzi uliofanywa miongoni mwa wazee ambao
walikuwa wanapata huduma ya bure ya kupima afya zao kwa msaada wa shirika
lisilo la kiserikali la The Good Samaritan Social Services umethibitisha
ubakaji na ndoa za utotoni ni matatizo makubwa maeneo ya Mlandizi na viunga
vyake.
Mkurugenzi wa Shirika hilo, Elisha Mwamkinga
alisema shirika lake linajitahidi kuwaelimisha wazee kuishi kwa heshima katika
jamii na kuepuka mambo ya aibu miongoni mwao.
Kwa ufadhili wa Shirika la HelpAge
International, zaidi ya wazee 300 wa Mlandizi walipima afya zao, na wengi wao wakapongeza
juhudi zinazofanya na shirika hilo katika kuwapa huduma mbalimbali za kiafya na
chakula.
No comments:
Post a Comment