Mkazi wa Kijitonyama, Dar es Salaam, Joseph Mumbi ambaye
alikamatwa na polisi Kisarawe akishukiwa kutaka kufanya uhalifu wa kutumia
bastola siku ya Ibada ya Ijumaa Kuu ilipokuwa ikiendelea katika Kanisa Katoliki
la Mtakatifu Stephano, ameachiwa jana kwa dhamana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema
Mumbi ameachiwa baada ya
Polisi kujiridhisha na maelezo ya awali aliyoyatoa
pamoja na kuwasilisha vielelezo
vilivyothibitisho uhalali wa umiliki wa silaha hiyo .
Hata hivyo, Kamanda Matei alisema pamoja na kupata
dhamana, polisi bado wanaendelea na uchunguzi ili kujiridhisha kama hakuwa na
nia mbaya.
Alisema madai kuwa alikuwa hatulii wakati wa misa pamoja
na kitendo chake cha kushika simu yake ya kiganjani mara kwa mara kama mtu
aliyekuwa akitaka kufanya mawasiliano kiasi cha kuwafanya waumini wamshuku kuwa
alitaka kufanya uhalifu, ndiyo yanayowafanya waendelee kumchunguza.
Kamanda Matei aliongeza kuwa, tayari simu ya mkononi
aliyokua akiitumia kwa mawasiliano siku hiyo imepelekwa Ofisi ya Kampuni ya
Tigo ili wafuatilie mawasiliano yaliyofanyika siku hiyo.
“Tigo wanafuatilia mawasiliano ya simu hiyo halafu
watatutaarifu ili nasisi tukamilishe uchunguzi wetu kuhusiana na jambo hili,”
alisema Kamanda Matei.
Mumbi alishukiwa kuwa huenda akawa ni mhalifu kutokana na
muonekano wake uliotia shaka.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment