Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sofia Mjema, amewataka
wazazi kuwa na tahadhari na ngoma za
vigodoro, chipsi kuku na simu za mikononi baada ya kuonekana kuwa vyazo vikuu
vya wanafunzi wa kike kukatisha masomo na kupata mimba.
Akizungumza katika
maadhimisho ya wiki ya elimu, Mjema
alisema anasikitishwa na baadhi ya wazazi wanaokwepa majukumu yao kwa
kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika vitendo hivyo na kusababisha elimu
kuporomoka.
Hata hivyo, aliwapongeza watendaji na wadau wa elimu kwa
jitihada zao za kuisaidia wilaya hiyo hadi mwaka huu kuwa ya kwanza mkoa wa Dar
es Salaam kwa kufaulisha wanafunzi zaidi ya asilimia 70 .
Maadhimisho hayo yaliyofanyika Kata ya Kijichi
yaliandaliwa pamoja na Manispaa Temeke, taasisi ya kijamii ya Ocode na Shirika la Kimataifa la We World
ambapo baadhi ya shule na wanafunzi waliofanya vizuri walipewa zawadi.
“Haiwezekani mtoto anatoka masaa matatu bila taarifa
halafu mnakuwa kimya, muda huo ni mwingi
kwa binti kuharibu maisha yake, ngoma za vigodoro na safari za ufukweni
si salama lazima tuhakikishe tunawajibika kuwakemea,” alisema Mjema.
Alisema mwaka huu waliamua kufanya kazi maalum kwa ajili
ya kuinua kiwango cha elimu ambapo matunda yake yameonekana baada ya ufaulu
kuongezeka kwa shule za msingi na sekondari.
Alisema ufaulu kwa shule za msingi ulikuwa asilimia 72
mwaka jana kutoka asilimia 60 mwaka 2003 na asilimia 64 kutoka chini ya
asilimia 50 kwa sekondari.
“Ufaulu huu umeonyesha jinsi tulivyoamua kuwa pamoja kati
ya serikali na wadau kuhakikisha elimu yetu inakua kwa kasi, nawapongeza na
nawataka kuongeza kasi zaidi ili tuongoze ngazi ya Taifa,” alisema.
Mratibu wa Ocode, Joseph Jackson, alisema kwa
kushirikiana na We World wametumia jumla ya Sh. milioni 655.9 kwa ajili ya
kuboresha mazingira na utendaji wa kazi ya walimu kwa shule nne za msingi.
Alizitaja shule zilizonufaika kuwa ni Kijichi, Bwawani,
Kibondemaji na Buza.
Alisema shule hizo zimeboreshwa kwa kukarabatiwa
madarasa, mitandao ya maji, jiko kwa ajili ya kupikia chakula cha wanafunzi
pamoja na ununuzi wa madawati kwa shule hizo.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment