Rais Jakaya Kikwete, amesema serikali haina nafasi za
ajira kwa sasa na kuwataka watu wasio na ajira kuelekeza nguvu zao katika sekta
binafsi.
Akihutubia sherehe ya
Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei
Mosi, iliyofanyika kitaifa jijini Mwanza jana, Rais Kikwete alisema kwa sasa
serikali yake haina matumaini ya kuwapa ajira wale wasio na ajira bali
wanachotakiwa ni kutegemea zaidi sekta binafsi.
“Matumaini ya kupata ajira serikalini kwa sasa hakuna,
bali kimbilieni katika sekta binafsi,” alisema Kikwete.
SEKTA BINAFSI
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema katika kipindi cha miaka
10 ya uongozi wake kinachomalizika
Oktoba, mwaka huu, serikali yake ilitoa ajira zaidi ya milioni mbili, miongoni
mwa hizo zaidi ya 600,000 zilitoka sekta za umma.
Alisema bado ukosefu wa ajira nchini ni tatizo kubwa na
licha ya utafiti mkubwa unaoendelea ili kuangalia soko la ajira, bado wananchi
wengi hawana ajira.
Alisema serikali yake ilifanikiwa kuboresha mishahara
katika sekta binafsi kutoka Sh.48,000 mwaka 2005 hadi kufikia 700,000 kwa
baadhi ya sekta binafsi.
“Wapo baadhi ya waajiri wanaolipa viwango visivyokubalika
mpaka sasa kwa wafanyakazi wao, ukiwauliza wanakupa visingizio vingi mara
uzalishaji umepungua,” alisema. Aidha, Rais Kikwete aliwapongeza wakaguzi wa
afya na usalama mahali pa kazi (Osha), kwa kufanikiwa kufanya kaguzi 56,000
pamoja na kaguzi maalum 26,000 nchini.
Alisema kutokana na kazi zinazofanywa na Osha, serikali
itaiimarisha ili iweze kufanya kazi kwa utendaji ulio bora zaidi.
WALIMU
Alisema muundo wa walimu umeidhinishwa na utekelezaji
wake umeanza Julai mwaka jana huku madai yao yakiwa zaidi ya Sh. Bilioni 53 kwa
serikali.
“Hawa walimu ambao ni shemeji zangu, wanatudai serikali
zaidi ya Sh. Bilioni 53 kwa ajili ya walimu 70,668 na tayari walimu 29,243
wamelipwa zaidi ya Sh. Bilioni 23,” alisema Rais.
Aidha, alisema madai ya walimu 30,807 ambao wanaidai
serikali zaidi ya Sh. Bilioni 17, baada ya uhakiki uliofanywa majina
yalionekana yana kasoro, lakini malimbikizo ya walimu
yanaendelea kufanywa na kulipwa kabla ya Agosti, mwaka huu.
Kadhalika alisema serikali inakusudia kuanzisha tume ya
watumishi ya walimu ili waweze kuitumia pamoja na bodi itakayowahusu.
KODI
Kuhusu kodi, alisema serikali yake inaendelea kujitahidi
kupunguza kodi ya mapato kwa wafanyakazi kama ilivyofanya kutoka asilimia 18.5
mwaka 2007 hadi asilimia 12 sasa.
“Jambo hili tunafahamu linawaumiza zaidi wafanyakazi,
lakini tutajitahidi katika bajeti ya serikali ya mwaka huu kupunguza tena ili
iweze kukaribia asilimia 9…serikali ijayo nayo kama itaamua kupunguza, itafanya
hivyo,” alisema.
Aliwaagiza makatibu wakuu wa wizara zote kuhakikisha
inawabana waajiri ambao hawajaunda mabaraza ya wafanyakazi kwa kipindi kirefu.
Alisema mabaraza hayo yanatakiwa kukutana mara mbili kwa
mwaka, na wala kusiwe na kisingizio cha kutokuwa na pesa za kukutana, kwani
mara nyingi pesa za vikao wanakuwa nazo.
Hata hivyo, alisema kabla hajang’atuka kutoka katika
uongozi Oktoba, mwaka huu, atahakikisha anakutana na mabaraza hayo lakini pia
atamshawishi Rais ajaye kuendelea na utaratibu huo wa kukutana na mabaraza ya
wafanyakazi. Aliongeza kuwa changamoto za wafanyakazi nchini haziwezi
kumalizika kwani hata marais waliotangulia akiwamo Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, hawakuweza
kumaliza kero za wafanyakazi nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
(Tucta), Nicholas Mgaya, alisema changamoto wanazokumbana nazo wafanyakazi ni
pamoja na makato makubwa ya kodi ambayo wanataka yapunguzwe hadi kufikia
asilimia 9.
Mgaya alisema hali hiyo imekuwa ikiwaumiza wafanyakazi
wengi hivyo inachotakiwa serikali kuangalia upya katika bajeti ya 2015/16 iweze
kupunguza.
Aidha, Mgaya alisema waajiri wengi wamekuwa wakiwatisha
wafanyakazi bila kuchukuliwa hatua yoyote ya kisheria, hali inayochangia
kuzorotesha uchumi.
Alisema mawakala wa ajira nchini wamekuwa wakifanya mchezo
kwa waajiriwa kutokana na kugeuka waajiri badala ya kazi yao, hivyo lazima
waajiwa wapewe kipaumbele kazini.
Aidha, kuhusiana na ajali zilizotokea nchini katika miezi
ya karibuni, Mgaya alisema serikali ichukue hatua stahiki kuweza kudhibiti
ajali hizo za barabarani, kwani uwajibikaji ukiwepo lazima zitadhibitiwa.
DK. SHEIN AAHIDI KULIPA MALIMBIKIZO
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia
watumishi wa umma kuwa serikali itawalipa malimbikizo ya madai yao yote mapema
mwaka wa fedha 2015/2016.
Akizungumza na wafanyakazi wakati wa maadhimisho ya Siku
ya Wafanyakazi Duniani jana yaliyofanyika katika viwanja vya Kiwanda cha
Mkonyo, wilaya ya Chakechake Pemba, Dk. Shein amewahakikishia watumishi hao
kuwa serikali inazifanyia kazi kasoro hizo na kuwahakikisha kuwa hakuna
mtumishi atakayepoteza haki yake.
Dk. Shein alibainisha kuwa hatua zote zinazochukuliwa na
serikali kuimarisha hali ya wafanyakazi, lengo lake ni kulifanya suala la
kuwapatia maslahi bora watumishi wa umma liwe endelevu kadri uchumi
unavyoimarika.
Miongoni mwa hatua hizo ni kupitisha sheria mbalimbali
zikiwamo Sheria Na. 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011.
Dk. Shein aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa Serikali ipo
katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya usalama kazini ili kuweka mfumo
mzuri wa afya katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwakinga wafanyakazi na
ajali na majanga mengine katika sehemu
za kazi.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment