Wakati wateja wa umeme wamendelea kutaabika, Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO), limetoa malekezo zaidi ya namna ya upatikanaji wa
huduma hiyo kwa urahisi.
Taarifa ya Tanesco imekuja baada ya tatizo lililojitokeza
kwa baadhi ya mawakala wa Luku kushindwa
kutoa huduma ya kuuza umeme na kusema
litamalizika karibuni.
Hali hiyo imetokana na Kampuni ya Selcom ambaye ni wakala
wa kuuza na kuziunganisha baadhi ya kampuni za simu kwa Tanesco kusitishiwa
huduma kutokana na kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu
yake ikiwamo kughushi nyaraka na kukiuka taratibu za kulipa kodi.
Taarifa iliyotolewa jana na shirika hilo, na kusainiwa na
Ofisa Habari wake, Adrian Severin ilisema kuwa huduma zinaendelea kupatikana
kupitia Kampuni ya MAXCOM katika Vituo mbalimbali, ATM za CRDB na NMB, NMB
Mobile pamoja na ofisi zote za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) nchi nzima
hadi siku ya Jumamosi na Jumapili na siku za Sikukukuu kuanzia saa 2:00 asubuhi
hadi saa 2:00 usiku.
“Shirika linaomba radhi kwa usumbufu wowote unaojitokeza,
wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa”alisema
Sevelin.
Wakazi wa Dar waonja joto ya jiwe
Gazeti hili lilizunguka katika vituo mbalimbali vya kutoa
huduma hiyo na kukuta misululu ya wananchi wakisubiri huduma hiyo huku kukiwa
na tatizo la mtandao.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti
katika vituo mbalimbali kikiwamo cha Kisutu, Kinondoni Mkwajuni, Buguruni
Sheli, Gongo la Mboto, Faya, Mwananyamala , Mwenge Mpakani, Kigogo, Tandale,
Mbagala Zakhem, walisema kuwa wamesimama katika foleni hizo kusubiri huduma
hiyo tangu saa 12 asubuhi.
Imelda Wahuzi aliyekutwa katika kituo cha Buguruni
alisema kuwa ameanza kupata adha hiyo tangu jana mchana , ambapo aliahirisha
kununua akiadhimia kudamka asubuhi ya leo, lakini anashangaa amefika kituoni
hapo saa 12asubuhi na hadi saa nne asubuhi hajapata umeme.
Muuza umeme katika kituo hicho ambaye alikataa kutaja
jina lake alisema kuwa pamoja na watu kuja kwa wingi kupata huduma hiyo katika
kituo hicho bado kuna tatizo la mtandao kusumbua ndiyo maana foleni inakuwa
kubwa.
Alisema kama siyo mtandao kusingekuwa na foleni, huku
akikiri kuwa hajawahi kuwa na watu wengi kama siku hizi mbili, yaani juzi na
jana.
Ibrahimu Hassan aliyekutwa katika foleni Kisutu alisema
kuwa amelazimika kusitisha shughuli zake baada ya siku iliyopita kupata hasara
kwa sababu hakufanya kazi katika kiwanda chake cha kuchomelea mageti kutokana
na kukosa umeme.
Alisema hajawahi kununua umeme katika foleni kiasi hicho
kwani hununua kwa njia ya simu, baada ya kupata ujumbe mfupi kutoka kwenye
mtandao wa simu kuwa hawezi kununua umeme kutokana na tatizo la kiufundi ndiyo
amefika katika kituo hicho.
Wakizungumza kwa jazba na mwandishi wa gazeti hili,
wateja waliokutwa katika kituo cha mafuta mpakani, walisema kuwa ni kero kwani
hakuna mwenye uhakika wa kupata umeme kwani kila saa mtandao unagoma.
“Hii nchi bwana kama imeuzwa, kila kitu shida, ukienda
benki foleni, hospitali, kwenye maji basi hata umeme, tumechoka jamani,
”alisema kijana wa makamo aliyejitambulisha kwa jina moja la Henry.
Kwa upande wa muuza umeme katika kituo cha Mbagala Rangi
Tatu, Hidaya Ussi alisema kuwa kila unapofika mwisho wa mwezi kunakuwa na adha
kama hiyo ya wateja kuwa wengi. “Hali hii ni kawaida kila mwezi huwa tunakutana
nayo, wateja wanakuwa wengi, lakini jana (juzi) na leo (jana) wamezidi kwa
sababu baadhi ya vituo vidogo vidogo vimefungwa hivyo wote wanakuja huku,
mtandao nao unachangia huduma kuwa ya taratibu, ”alisema Ussi.
Selcom waiangukia Wizara
Mkurugenzi Mtendaji wa Selcom, Sameer Hirji, amemuomba
Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene aingilie kati mgogoro wao na
Tanesco ili waendelee kutoa huduma, huku akifafanua tuhuma zilizotolewa dhidi
yao juu ya kukiuka kulipa kodi. Selcom ilisitishiwa kutoa huduma kwa kile
kilichoelezwa kukwepa kodi.
Taarifa ya mkurugenzi huyo kwa vyombo vya habari jana
ilisema kuwa lengo lao siyo kuharibu huduma bali kuziboresha hivyo Waziri kwa
kutumia mamlaka yake anaweza kuumaliza mgogoro huo.
“Kwa kuzingatia makubaliano yetu na Tanesco juu ya uuzaji
wa Luku tumekuwa wahanga wa mara kwa mara kwa jambo hili kwa kuliweka wazi hili
Selcom haiwajibiki kwa TRA. Utaratibu wa mauzo ya Luku kama ulivyoanishwa chini
ya sheria ya mwaka 2011 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) Tanesco ndiye
mmiliki halali husika wa bidhaa na siyo msambazaji wa huduma,, ” ilisema
taarifa hiyo.
Hata hivyo, jana mchana Selcom iliwatumia ujumbe mfupi
mawakala wao kuwaomba radhi kutokana na usumbufu uliojitokeza
“Tuomba radhi kwa usumbufu mnaopata kutokana na tatizo la
Luku, juhudi zinafanyika kuhakikisha huduma hii inaanza kufanya kazi haraka
iwezekanavyo asante,” ulisomeka ujumbe huo.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment