Mtanzania aliyekamatwa Kenya akidaiwa
kufanya ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa uliosababisha vifo vya watu 148,
Rashid Charles Mberesero (20) ni mwanafunzi wa kidato cha tano, lakini uongozi
wa shule anayosoma umesema alitoweka shuleni hapo Desemba mwaka jana.
Mama mzazi wa kijana huyo, Fatuma Ali alisema jana kuwa:
“Baada ya kufaulu alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya Bihawana na likizo
alirudi nyumbani na baada ya likizo kuisha aliniaga anarudi shuleni.”
Taarifa hizo zimekuja wakati Mberesero maarufu kwa jina
la Rehani Dida, akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo jijini Nairobi baada ya
watuhumiwa wengine kufikishwa mahakamani juzi.
Mwendesha mashtaka, Daniel Karuri alisema, “Rehani Dida”
hakufikishwa kortini kwani alikuwa na wapelelezi mjini Garissa kukusanya
ushahidi zaidi, baada ya kukiri kuwa ni mfuasi wa kundi la Al-Shabaab.
Mtanzania huyo anadaiwa kukamatwa baada ya kujificha kwa
saa nane akiwa amejichanganya na maiti, lakini baadaye alipanda na kujificha
darini akiwa na mabomu.
Kauli ya wazazi
Jana, mama huyo, aliliambia gazeti hili kuwa haelewi ni
nani aliyemshawishi mwanaye kujiunga na kundi hilo na kwamba jambo hilo
limemshtua.
“Hizi taarifa tumezisikia na kuona kwenye TV na kwa kweli
zimetushtua sana, mimi nahisi huko shule ndiko alikokutana na watu wabaya,”
alisema Fatuma ambaye ni mkazi wa Gonja wilayani Same.
Baba mzazi wa mtuhumiwa huyo, Charles Mberesero Temba,
alikiri kuwa Rashid ni mtoto wake ambaye alizaa na Fatuma mwaka 1994 na miaka
yote alikuwa akiishi na mama yake.
“Huyo mtoto sijawahi kuishi naye, muda wote tangu 1994
alikuwa akilelewa na mama yake,” alisema Temba na kuongeza kuwa hakuwahi kuishi
na mzazi mwenzake huyo.
“Mwaka jana mama yake ndipo alinikutanisha na mtoto na
akanitambulisha na mimi nikamshauri abadili dini kwa sababu mimi ni Mkristo
Mkatoliki,” alisema.
Alisema aliendelea kuwasiliana naye na aliwahi kumpeleka
kanisani mara tatu akimshauri abadili dini ili arudi kwenye dini ya baba,
lakini alikataa.
Alisema inavyoonekana ushauri wake huo haukupokewa vizuri
na mwanaye na huyo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mawasiliano baina yao kukatika.
Kutoka Bihawana
Habari zilizopatikana jana kutoka shuleni Bihawana
zilisema kuwa Mberesero alitoroka shuleni Desemba mwaka jana, baada ya kukaidi
kuvua kofia katika eneo la shule.
Mkuu wa Shule hiyo, Joseph Mbilinyi alisema alimpokea
mwanafunzi huyo Agosti 15, mwaka jana akitokea katika Shule ya Sekondari ya
Kigwe wilayani Bahi.
Alisema mwanafunzi huyo alipata uhamisho baada ya
kubadilisha masomo kutoka masomo ya sanaa mchepuo wa Historia, Jiografia na
Kiswahili (HGK) na kuingia katika masomo ya sayansi ya Fizikia, Kemia na
Biolojia (PCB).
Mbilinyi alisema katika shule hiyo wanafunzi walikuwa na
mazoea ya kuvaa rozali na kofia, jambo ambalo alilipiga marufuku lakini Novemba
24, mwaka jana alikutana na kijana huyo akiwa amevaa kofia.
“Nilimwambia aivue aichanechane mbele yangu, lakini
alikataa na kunijibu kuwa amezoea kuivaa na hawezi kuichana. Kwa sababu ilikuwa
ni usiku niliondoka na kofia hiyo na kumwambia kesho yake asubuhi aje ofisi
kwangu ili tumalize suala hilo, alikuwa ni mtu wa kwanza kufika ofisi kwangu.
Nilimwambia anieleze kwa nini hataki kuichana, ningeweza kumsaidia kumtafutia
shule ambazo zinaruhusu mavazi hayo.”
Alisema hata baada ya mazungumzo hayo, Rashid hakueleza
kwa nini alikataa kuichana ndipo alipoambiwa kuwa angerejeshwa nyumbani ili aje
na mzazi wake na aichane mbele yake.
“Kwa kawaida wanafunzi wengine ukiwaeleza hivyo, huwa
wanaomba msamaha yanaisha lakini kwa Rashid ilikuwa ni tofauti, aliniambia yuko
tayari kurudishwa nyumbani lakini siyo kuchana kofia hiyo,” alisema.
Mwalimu huyo aliongeza: “Niliona njia ya kumsaidia ni
kuwashirikisha walimu ambao wanasimamia msikiti wetu huu. Walimu walimuita na
akakubali kupewa adhabu ili jambo hilo liishe bila kufikishwa kwa wazazi wake.”
Hata hivyo, alisema baada ya mazungumzo hayo, Rashid
alichukua begi lake na kuondoka kwenda mjini na kuwaacha wenzake wakimalizia
mtihani wa Biolojia.
“Nilipata shida sana sikupenda mwanafunzi huyu aondoke
shuleni, nilitaka hili jambo lipate suluhu. Nilipigia simu alizoandikisha shule
ikiwamo ya baba yake bila mafanikio kwa sababu hazikupokewa, isipokuwa moja
ambayo ilipokelewa na mwanamke ambaye alikana kumfahamu.
“Hadi leo bado ni mwanafunzi wetu kwa sababu kanuni
zinasema baada ya siku 90 kama mwanafunzi hajaonekana shuleni, tunapeleka jina
kwenye Bodi ya Shule ambayo itatoa uamuzi,” alisema.
Katibu mstaafu wa Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu katika
shule hiyo, Mungi Ramadhan Mungi alisema Rashid alikuwa ni mtu wa msimamo,
akitaka jambo lake hata kama halina usahihi analisimamia.
“Aliwahi kutaka kupigana msikitini mara mbili, mara ya
kwanza tulikuwa tukiuliza maswali kuhusu masomo ya darasani yeye akasema
hairuhusiwi kufanya hivyo msikitini,” alisema.
Alisema hatua hiyo ilizua mabishano na alifikia uamuzi wa
kutaka kuwachapa walioongelea mambo ya masomo ndani ya msikitini.
“Alikuwa ni mtu wa msikitini na bwenini mara nyingi
hakupenda kuchanganyika na wenzake, jambo hilo lilimfanya hata kukosa
marafiki,” alisema.
Alisema aliwahi kuwahadithia kuwa alibadili dini akiwa
anasoma sekondari huko Moshi.
Mwalimu anayewasimamia wanafunzi wa Kiislamu, Mohamed
Mwijuma alisema baada ya Rashid kutoroka shuleni hapo waligundua alikuwa ni
mwanafunzi aliyekuwa na matumizi yasiyo ya kawaida.
“Pia tuligundua kila mwisho wa wiki alikuwa akitoroka
kwenda mjini,” alisema Mwijuma ambaye alishiriki kulipatia ufumbuzi tatizo hilo
la kukutwa na kofia shuleni.
Hata hivyo, alisema Februari mwaka huu, Rashid alirejea
mwisho wa wiki na kuondoka moja kwa moja na mizigo yake yote.
Habari zilizopatikana shuleni hapo zilisema baada ya
Rashid kutajwa kuhusika na tukio hilo, mama yake mzazi alifika shuleni hapo
kumtafuta mwanaye.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment