MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuamuru
Mbunge wa Jimbo la Dimani Zanzibar, Abdallah Sharia Ameir (CCM) kutoa Sh
200,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto wake wa kiume, mwenye umri wa
miaka mitatu na nusu, anayedaiwa kumtelekeza.
Pia, aliamuru mtoto huyo kulelewa na wazazi wake
na siyo bibi yake, kama alivyokuwa akitaka mbunge huyo. Hivyo ataendelea kukaa
na mama yake.
Kwa upande wake, Wakili Gideon Mandes aliyekuwa
akimtetea Hawa Deus aliyekuwa mke wa mbunge huyo, alisema kupitia hukumu hiyo
Mahakama imetoa uamuzi wa haki.
“Kupitia hukumu hii nimebaini wazazi wanawajibu
wa kumtunza mtoto wanayemzaa bila ya kujali hali yake hata kama ni ya ulemavu
asitelekezwe na imedhihirisha hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba sheria
ipo sawa kwa kila mtu,”alisema wakili huyo.
Wakili huyo aliwashauri Watanzania wenye
matatizo na changamoto kama hizo, kuweka bidii ya kuijua sheria na taratibu
zake ili waweze kuitumia kupata haki na suluhisho kupitia Mahakama.
Mwezi Januari 2015, Hawa alivamia kikao cha
Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala akiwa amesindikizwa na kundi la
watu, ambao mmoja wao alikuwa amembeba mtoto wa mbunge huyo mwenye ulemavu,
huku wakipiga kelele na kuwaacha wabunge na viongozi wa dini waliokuwepo
kupigwa na butwaa.
Mtafaruku huo ulitokea katika ukumbi wa mikutano
wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, ambapo kikao hicho kilikuwa
kinaendelea na mjadala kuhusu marekebisho ya Muswada wa Sheria ya
Kiislamu.
Miongoni mwa kundi waliomsindikiza Hawa ni
mwanaharakati Joyce Kiria, na watu wengine ambao hawakufahamika mara moja.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment