Takribani siku 22 zikiwa zimepita tangu madereva wagome
kutoa huduma za usafiri nchi nzima, leo wametangaza mgomo mwingine kutokana na
ukimya dhidi ya madai yao kwa serikali.
Madereva hao jana walitoa tamko la
kuwapo kwa mgomo huo kupitia vyama vyao, huku
wakikanusha kwamba watagoma sambamba na kuandamana.
Walisema leo watakuwa kwenye ofisi zao za muungano wao
zilizopo Ubungo, jijini Dar es Salaam na hawatatoa huduma za usafiri.
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Umoja wa Madereva
na Chama cha Malori, Rashid Salehe, alisema, mgomo upo pale pale kwa madai kuwa
bado kuna mambo ambayo yameendelea kuwa kikwazo kwao.
Alisema iwapo serikali haitatoa majibu ya kuridhisha, leo
hawataingia barabarani kutoa huduma za usafiri.
Alisema jana walifanya mkutano wa madereva jijini Dar es
Salaam huku ajenda kubwa ikihusu mgomo huo.
Alitaja baadhi ya sababu zinazowafanya wagome kwa mara
nyingine kuwa ni serikali kutotekeleza madai yao likiwamo la kupewa ajira rasmi
na waajiri wao.
“Msimamo wetu upo palepale kwamba kesho (leo)
hatutaendesha magari..madereva wanaambiwa wezi, tunataka mikataba
iboreshwe…tutakaa hapa hata ndani ya
siku saba hadi serikali ije na kutoa
majibu yanayoridhisha. Tunataka tupatiwe mikataba inayoeleweka na waajiri wetu
mbele ya serikali,” alisema na kuongeza:
“Tumekaa katika kikao cha leo (jana) kwa ajili ya
kuangalia maazimio ya kikao tulichokaa Aprili 29, mwaka huu…katika kikao hicho
zaidi ya madereva 40 walisema hawana hela.”
TABOA WAIPA
ANGALIZO SERIKALI
Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa),
Enea Mrutu, alisema walipata taarifa zote kuhusu mgomo huo na kueleza kwamba
wanaotangaza mgomo huo siyo madereva walioajiriwa.
Kwa mujibu wa Mrutu, madereva hao ndiyo waliosababisha
magari yao kutoingia barabarani Aprili 11, mwaka huu na kuitaka serikali
kuingilia kati suala hilo, vinginevyo leo magari hayataweza kuingia barabarani.
DARCOBOA: MGOMO
UWE WA HIARI
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam
(Darcoboa), Sabri Mabrouk, alisema chama hicho kina taarifa kuhusu mgomo huo,
lakini akaeleza kusikitishwa kwake kwa namna madereva wa vyombo vya usafiri
wanavyowahusisha wao akisema hawahusiki.
Kutokana na hilo, Mabrouk aliomba mgomo huo usiwe wa
lazima bali wa hiyari kwani si vyema kuwahusisha wao wanaohusika na daladala
tena ndani ya mkoa na kupewa vitisho vya kupigwa mawe endapo gari lolote
litakaidi agizo hilo.
“Serikali iangalie suala hili, kama kuna jambo lipo nyuma
ya pazia basi liwekwe wazi….kama ni wa mikoani kwa nini wanatuhusisha sisi,
tusitafute kuwasumubua wananchi,” alisema mwenyekiti huyo wa Tarcoboa.
SUMATRA: WANANCHI WATASUMBULIWA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa
Nchikavu na Majini (Sumatra), Gilliard Ngewe, alisema, suala hilo lipo katika
wizara husika na kwamba kufanyika kwa mgomo huo kutaathiri wananchi kutokana na
kukosa huduma za usafiri.
Hata hivyo, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Uchukuzi,
Samuel Sitta (pichani), bila mafanikio kutokana na simu yake kutopatikana, huku
Naibu wake, Charles Tizeba, akisema: “Naomba mnitafute kesho..nipo msibani.”
NIPASHE pia lilimtafuta Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudensia Kabaka na Naibu wake, Makongoro Mahanga, lakini simu zao hazikuwa
hewani.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga,
alikaririwa na vyombo vya habari juzi akisema
amepokea ujumbe mfupi wa simu kwamba leo kuna mgomo.
Tishio la mgomo wa leo ni mwendelezo wa mgomo mwingine
mkubwa ambao ulidumu kwa takribani saa saba kwa mabasi kutokuruhusiwa kutoka
katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Ubungo,
Aprili 11, mwaka huu.
Madai ya mgomo huo ambao ulileta adha kubwa kwa wananchi
yalikuwa ni kupinga ucheleweshwaji wa malori kwenye mipaka hususani ya Tunduma
ambako hukaa kwa zaidi ya siku 26 licha ya kulipiwa kila kitu bandarini.
Mengine ni kupinga sheria namba G 31 ya mwaka 2015
ambayo inazungumzia faini ya Sh. 300,000 au kifungo cha miezi 21 kwa madereva
wanapofanya makosa barabarani. Pia kupinga madereva kutakiwa kwenda Chuo cha
Taifa cha Usafirishaji (NIT) kila baada ya miaka mitatu kwa ajili ya kujinoa.
Madai mengine yalikuwa ni
wamiliki wa magari kutowashirikisha madereva katika mikataba yao ya
kazi.
Hata hivyo, mgomo
huo ulisitishwa baada ya serikali kupitia kwa Waziri Kabaka kufuta sharti la
kwenda chuoni kila baada ya miaka mitatu.
Pia aliahidi kulipatia ufumbuzi suala la mikataba yao katika kikao kilichotarajiwa
kufanyika wiki iliyofuata.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment