Monday, April 13, 2015

Mama Mzazi wa Rashid Mberesero Anataka Kwenda Kumwona Mwanaye....Jeshi la Polisi Halina Uwezo wa Kumsaidia Kutokana na sheria mpya za Ugaidi za Kenya...Awali Mama huyo Alijua Rashid yuko Shuleni

RASHID MBERESERO
WAKATI mama mzazi wa Mtanzania Rashid Mberesero anayetuhumiwa kuwa kati ya wafuasi wa Al-Shabaab walioua wanafunzi 148 wa Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya akitaka msaada wa Serikali ili akamwone mwanawe huyo, Jeshi la Polisi limesema halina uwezo wa kumsaidia.

Jeshi hilo limesema halina uwezo wa kumsaidia mama huyo, Fatma Ally kutokana na sheria mpya za ugaidi zilizopitishwa nchini Kenya hivi karibuni na kuwekewa pingamizi mahakamani.

Aidha limesema kadi sasa bado halijafuatilia tukio la kukamatwa kwa kijana huyo na kuwa habari zake linazifuatilia kwenye vyombo vya habari tu.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja, ameliambia MTANZANIA kuwa hajui msimamo wa Kenya ukoje kuhusu tukio hilo.

Alisema suala hilo ni la kisheria zaidi na sheria zinatofautiana baina ya nchi na nchi ikiwamo utaratibu wa kumwona mtu akiwa mahabusu.

“Jeshi la Polisi hatujui chochote kuhusu mtuhumiwa huyo zaidi ya kusoma kwenye magazeti, kwa hiyo ni ngumu kusema kama mama yake ataweza kumwona au la kutokana na sheria mpya za ugaidi walizopitisha wenzetu hivi karibuni.

“Sijazipitia vizuri sheria hizo, lakini baadhi yake zina makali zaidi, kwa hiyo siwezi kutia neno, tuwaachie uhuru wa sheria zao wenzetu waamue,” alisema.

Aidha alipoulizwa kuhusu taarifa za utaratibu wa kijana huyo kuwepo nchini Kenya, alisema hawana taarifa zake zaidi ya kusoma kwenye magazeti kwamba alitoweka nyumbani na shuleni.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali sasa inategemea huruma ya Kenya katika kumponya ama kumwadhibu kijana huyo kwa mujibu wa sheria zake.

Kwa mujibu wa Fatma alikuwa anajua mtoto wake yupo shuleni Bihawana mkoani Dodoma alipokuwa akisoma kidato cha tano huku uongozi wa shule ukisema alitoroka tangu Novemba mwaka jana.


Sheria mpya ya ugaidi nchini Kenya, ambayo baadhi ya vipengele nane vilipingwa mahakamani inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya dola 55,000 kwa uchapishaji bila ruhusa wa makala au kutafuta habari amzazo zitatatiza uchunguzi ao operesheni ya kupambana dhidi ya ugadi.

No comments:

Post a Comment