Siku moja tu baada ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk.
Reginald Mengi, kutangaza usalama wa maisha yake kuwa hatarini, kiongozi wa
Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameibuka na kudai tuhuma alizohusishwa
dhidi ya Mengi si za kweli.
Zitto alihusishwa katika habari hiyo kuwa ndiye
anayedaiwa kwenda kwa Rais Kikwete kumweleza kuwa Mengi anaihujumu serikali yake baada ya
kutolewa kwa ripoti ya PAC.
Alisema taarifa maalum ya Kamati ya Bunge Hesabu za
Serikali (PAC), kuhusu ufisadi wa Sh. Bilioni 306 za Escrow, haihusiani kwa
namna yoyote na Dk. Mengi.
Zitto alisema kuwa watu wanaomhusisha mfanyabiashara huyo
na mkakati wa kuihujumu serikali ya Rais Kikwete ni wale waliokosa hoja baada
ya masuala yao ya kuwahujumu Watanzania kukwama kufuatia ripoti ya PAC kuwaumbua.
Zitto alitoa kauli hiyo jana katika uwanja wa mahakama ya
Mwanzo mjini Shinyanga.
Katika hofu yake, Dk. Mengi alisema ameshangazwa na
ukimya wa Ikulu na Idara ya Habari Maelezo, pamoja na habari hiyo kuchapishwa
kwenye gazeti ikimhusisha Rais.
"Mengi sio
mbunge, sio mjumbe wa PAC na hakushawishi PAC kwa namna yeyote ile. Wezi wa
Escrow wasitapetape kutafuta mchawi wakati mchawi ni wizi wao wenyewe,"
alisema Zitto.
"Habari zilizoandikwa kwenye gazeti la Taifa Imara
zinazomhusu Regnald Mengi na Rais Jakaya
Kikwete si za kweli, ni fitina zimetengenezwa," alisema.
Zitto, aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC, alisema habari
iliyoandikwa na gazeti la Taifa Imara la Machi 23, mwaka huu, zinazoonyesha
kuwa alikutana na Rais kwa msaada wa watu mbalimbali, ni mwendelezo mwingine wa
porojo za watu walioathiriwa na uamuzi wa PAC katika sakata la Escrow.
"Habari hiyo ilibeba maudhui ya 'post' iliyoandikwa
katika mtandao wa Mwanahalisi online, inaonyesha kuwa mimi nilikutana na Rais
kwa msaada wa watu mbalimbali na katika kikao hicho inadaiwa nilisema kuwa
Mengi ndiye aliyechochea wabunge kuishughulikia serikali ya Rais Kikwete ili
ianguke,” alisema.
Zitto alisema hahitaji
kutumia watu kwa ajili ya kukutana na Rais Kikwete, kwa kuwa suala hilo
linawezekana kufanyika katika taratibu za kawaida za kiserikali.
Alisema kitendo cha gazeti hilo kudai kuwa aliomba watu
wamkutanishe na Rais, inaonyesha namna mwandishi alivyoshindwa kutunga uongo
wake.
“Hadithi ya kwamba nimeomba watu wanikutanishe na Rais
inaonyesha namna mwandishi alivyoshindwa kutunga uongo wake.
Katika kukutana kwangu na Rais kikazi sijawahi hata mara
moja kuzungumzia watu. Hivyo kusema nilikwenda Ikulu kumzungumzia Mengi ni kunidharau na kuidhalilisha Taarifa
ya Urais,” alisema.
Alisema ifahamike kuwa gazeti la Taifa Imara linamilikiwa
na James Rugemalira wa kashfa ya Escrow na kuendeshwa na Prince Bagenda,
aliyeandaa mkutano wa mmoja wa mawaziri waliofukuzwa kazi kwa kashfa hiyo.
Aliongeza kuwa hata chanzo cha habari hiyo ni mtandao wa
Mwanahalisi online ambao unaoendeshwa na mmiliki wa Mawio, gazeti ambalo kila
wiki lina habari za kutunga dhidi yake na chama chake.
Aidha, alisema kama kuna mtu ana chembe ya ushahidi wa
jambo hilo apeleke kwenye vyombo vya dola kwa hatua kuliko kurudia rudia porojo
hizo kwenye vyombo vya habari.
Alisema kwa sababu hiyo amemwelekeza mwanasheria wake
achukue hatua za kisheria dhidi ya gazeti la Taifa Imara na gazeti la Mawio,
kwa mfululizo wa habari za kutunga uongo dhidi yake kila kukicha.
Juzi Mengi alitoa
taarifa katika vyombo vya habari akielezea hofu yake juu ya ukimya wa Kurugenzi
ya Mawasiliano Ikulu, pamoja na Idara ya habari maelezo kufuatia taarifa
iliyoandikwa na gazeti la Taifa Imara la Machi 23 mwaka huu.
NIPASHE Jumapili alizungumza kwa njia ya simu na Mkurugenzi wa Habari
Maelezo, Assah Mwambene, na kujibu kwa mkato "no comment my dear" (sina
cha kuzungumza).
NIPASHE ilipowasiliana kwa njia ya simu na Katibu
Kiongozi wa Ikulu, Balozi Ombeni Sefue, alisema haelewi chochote kuhusu tuhuma
hizo na kujibu kwa mkato “no comment”.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment