NIANZE kwa kutoa pole kwa wadau wote wa muziki wa kizazi
kipya, kwa kuondokewa na mdau Abdul Bonge, muanzilishi wa Kundi la Tip Top
Connection, wale vijana wenye maskani yao pale Manzese.
Baada ya pole hiyo, kwa wasanii, wadau na jamii yote,
sasa nirejee kwenye mada yangu ambayo nazungumza na staa wa Bongo Fleva aliye
katika levo za juu kabisa, Diamond Platnumz.
Hivi karibuni kulikuwa na habari zilizosema kuwa msanii
huyo amehamia katika nyumba yake ya bei mbaya aliyoijenga huko Madale, nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Kabla ya kuhamia, kama walivyo vijana wengi wa
sasa, ‘alitupia’ picha kadhaa katika akaunti yake kwenye mtandao wa Instagram
akionyesha sehemu mbalimbali za nyumba hiyo ya kisasa.
Alionyesha bwawa la kuogelea, samani zilizopo sebuleni na
jikoni kwake sambamba na vitu vingine vilivyoendana na jumba lake hilo. Lakini
katika hali ya kushangaza, siku chache baadaye alisikika akisema kutokana na
ukubwa na thamani ya nyumba yake, vinamfanya ahofie maisha yake, hasa nyakati
za usiku anaporejea kutoka kazini au matembezini (Wasanii mara nyingi hufanya
kazi usiku).
Kwanza nimpongeze sana Diamond kwa kufanikiwa kumalizia
nyumba yake maana vijana wengi wa umri wake, bado wanaishi kwa wazazi wao.
Lakini wakati nikimpongeza, napenda pia kumshauri kuwa hivi sasa ameshakua
mkubwa, siyo tu kiumri, bali hata kiakili, kiasi kwamba anapaswa kuacha kufanya
baadhi ya mambo ambayo kimsingi, yanapishana naye.
Hatari anayoihisi kule nyumbani kwake alikojenga,
ameitengeneza mwenyewe. Ujana na ukisasa, unamfanya kuweka picha za baadhi ya
vitu vilivyomo ndani ya nyumba yake, jambo ambalo siyo baya, lakini unapoishi
na jamii iliyokata tamaa kama yetu, siyo jambo zuri.
Nchi yetu ina vijana wengi wasio na ajira, ambao wamekosa
fursa na bahati mbaya, wengi wao hawana elimu ya kutosha. Matokeo yake wanaishi
kwa kubangaiza ilimradi siku zinakwenda. Wakati Diamond ana uwezo wa kujenga
nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 400, wenzake wengi hawana hata uhakika
wa mlo wa siku.
Aina ya maisha ya Diamond, yanashawishi watu kudhani ni
tajiri sana, mwenye uwezo mkubwa kimaisha na hivyo ni kijana anayenuka fedha.
Kama nilivyosema, anaweza kuwa ni shabiki wa wengi, lakini unapofikiria kuhusu
tabu za maisha, watu hawaoni hatari kumdhuru ilimradi kama wana uhakika kuwa
watapata kitu cha kuwapunguzia ukali wa maisha.
Nadhani huu ni wakati wa Diamond kupunguza maisha ya
video. Ni haki yake kuamua chochote kinachomhusu, lakini busara haishawishi mtu
kutangaza unachomiliki pasipo sababu za msingi. Binafsi ninawajua wasanii wengi
ambao ‘wako vizuri’ kimaisha, lakini huwezi kuwadhania ukiwaona.
Yapo baadhi ya mambo tunayafanya kwa sababu ya umri,
ambayo kadiri tunavyokua hatuwezi kufanya. Wabongo hawajui kuwa unaweza kuwa na
nyumba kubwa, lakini usiwe na fedha ndani, watakuja na mapanga yao kulazimisha
uwape fedha, wasipopata utaambulia majeraha.
Ni kweli hata mastaa wa Ulaya wanaanika wanachomiliki,
lakini tambua kuwa ipo tofauti kubwa kati yetu. Wewe bado ni kijana mwenye
ndoto nyingi, acha matangazo, timiza ndoto zako!
Chanzo GPL
No comments:
Post a Comment