WATOTO 140 wenye umri kati ya miaka 10 na 21 wamekamatwa
wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wakilelewa katika misikiti mitatu tofauti.
Taarifa zilizopatikana wilayani hapa zinasema watoto hao
wamekuwa wakifundishwa mafunzo ya dini ya kiislam kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watoto hao waligundulika
baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Hai kupata taarifa na
kuwafuatilia kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kati ya Machi 25 na 27 mwaka
huu.
Taarifa hizo zimeyataja maeneo waliyokutwa watoto hao
kuwa ni Misikiti ya Masjid Bilal, Masjid Othiman na Msikiti wa Kwa Kiriwe.
Taarifa hizo zimesema katika Msikiti wa Masjid Bilal uliopo
Mtaa wa Kibaoni wilayani hapa, walikutwa watoto wa kiume 70 wanaotoka katika
mikoa mbalimbali nchini.
Watoto wengine 50 wa kiume walikutwa katika Msikiti wa
Masjid Othiman uliopo Mtaa wa Uzunguni ambao nao inasemekana wamekusanywa
kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa hizo zinasema watoto wengine 27 walikutwa katika
Msikiti wa Kwa Kiriwe ambako pia walikuwa wakifundishwa mafunzo ya dini ya
kiislam na walimu Watanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Anthoy Mtaka, alikiri kuwapo
watoto hao wilayani kwake.
“Tukio hilo lipo na wanaohusika ni watu wanaotumia
mwamvuli wa dini fulani kufanya mambo yasiyofaa katika jamii.
“Kwa hiyo naziomba mamlaka husika likiwamo Baraza Kuu la
Waisalam Tanzania (BAKWATA) kutambua miskiti na shughuli zinazoendelea katika
nyumba hizo za ibada.
“Hili lazima walifanyie kazi kwa sababu hao vijana
inasemekana wanafundishwa mazoezi makali ya kareti na judo katika nyumba hizo
za ibada,” alisema Mtaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela,
alisema atazungumzia tukio hilo leo.
Kupatikana kwa watoto hao ni mwendelezo wa matukio ya
watoto wanaolelewa kinyume cha sheria mkoani Kilimanjaro baada ya matukio
mawili ya aina hiyo kuripotiwa hivi karibuni.
La kwanza lilihusisha watoto 18 na la pili lilihusisha
watoto 11 waliokutwa katika maeneo ya Lyamungo wilayani Hai.
CHANZO: MTANZANIA
No comments:
Post a Comment