Ijumaa Kuu ni siku ya mwaka ambayo wafuasi wengi wa Yesu
Kristo wanaadhimisha kifo chake msalabani ambacho kilitokea nje ya kuta za mji
wa Yerusalemu siku ya Ijumaa.
Kadiri ya Mtume Yohane kesho yake ilikuwa Sabato na pia
Pasaka, jambo lisilotokea kwa kawaida. Kwa sababu hiyo wataalamu mbalimbali
wanakadiria ilikuwa tarehe 7 Aprili 30.
Ijumaa kuu ni sehemu ya Juma Kuu linaloanza kwa adhimisho
la Yesu kuingia mjini Yerusalemu akishangiliwa kama mfalme wa Wayahudi (yaani Masiya au
Kristo). Adhimisho hilo linafanyika mwanzoni mwa wiki, yaani Jumapili ya
matawi.
Ijumaa kuu pia ni sehemu ya siku tatu kuu za Pasaka
zinazoadhimisha mateso na kifo chake, kulala kaburini, na hatimaye kufufuka kwa
utukufu.
Siku tatu kuu za Pasaka ndizo kiini cha mwaka wa Kanisa.
Zinamuadhimisha Yesu mteswa, mzikwa na mfufuka, yaani
siku ya kwanza (Alhamisi kuu jioni hadi Ijumaa kuu jioni) inaadhimisha mateso
yake kuanzia karamu ya mwisho hadi kifo cha msalaba; siku ya pili (Ijumaa kuu jioni
hadi Jumamosi kuu jioni) inaadhimisha maiti yake kubaki kaburini na roho yake
kushukia kuzimu; siku ya tatu (kuanzia Jumamosi kuu jioni hadi Jumapili ya
Pasaka jioni) inaadhimisha ufufuko wake mtukufu.
Siku hizo tatu ni kama bawaba kati ya Kwaresima na
kipindi cha Pasaka.
Chanzo: Dewji blog
No comments:
Post a Comment