MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amemwandikia
barua Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akimtaka afike
mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa mahojiano.
Inaelezwa kuwa
Makonda alimtumia Askofu Gwajima barua hiyo Machi 30 mwaka huu, akiwa amelazwa
katika Hospitali ya TMJ. Hata hivyo, kiongozi huyo wa kiroho amegoma akisema
hawezi kwenda ofisini kwa mkuu huyo wa wilaya kwa mahojiano.
Mmoja wa wasaidizi
wa Askofu Gwajima aliliambia MTANZANIA jana kuwa hatua ya Makonda kumtumia
barua haikumpendeza kiongozi huyo wa kanisa.
“Makonda alikuja katika Hospitali
ya TMJ na kudai amekuja kumwona Askofu Gwajima huku akiwa amebeba barua yake.
Baada ya kumwuliza hali ya maendeleo ya afya yake alitoa barua na kumkabidhi
jambo ambalo halikuwa jema. “Baada ya muda Askofu Gwajima alituita wasaidizi
wake na kutueleza kuwa amepewa barua ya wito kwa DC, sasa tukajiuliza askofu
anaumwa. Je, inakuaje aende tena katika mahojiano na mkuu wa wilaya? “Na kama
ni hivyo nini kazi ya polisi maana wamemuhoji tangu siku ya kwanza baada ya
kumkamata. Je, inakuaje tena Makonda alete barua ya kumtaka askofu akahojiwe
tena mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya mbele ya DC?
“Hapa kuna
mchezo unataka kufanywa na je, katika masuala haya ya usalama sijui kama huyo
DC anajua wajibu wake. Mtu anahojiwa na polisi sasa inakuaje tena aitwe na DC
ahojiwe na kamati ya ulinzi?
Amesema hatokwenda,” alisema msaidizi huyo wa
Gwajima ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini. MTANZANIA ilimtafuta Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda kupata ufafanuzi wa barua yake hiyo, ambapo
alijibu kwa kifupi kuwa ni kweli amemwandikia barua ya wito kiongozi huyo.
Alipoulizwa ni hatua zipi Askofu Gwajima atachukuliwa kwa kutaa kutii wito huo,
Makonda alisema. “Kuhusu hatua subirini mtaziona wenyewe” alisema mkuu huyo wa
wilaya. Gwajima kuripoti polisi wakati huohuo, Askofu Gwajima leo anatarajiwa
kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea
kuhojiwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Gwajima aliachiwa kwa dhamana juzi
baada ya kutoka katika Hospitali ya TMJ ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu
baada ya kuanguka ghafla wakati akihojiwa na polisi.
Akizungumza na MTANZANIA
jana, Mwanasheria wa Gwajima, John Mallya alisema baada ya kuruhusiwa juzi, leo
anatakiwa kuripoti tena katika kituo hicho kuendelea na mahojiano. “Polisi
walituambia twende kesho (leo) kwa mahojiano kwa sababu yalikuwa
hayajakamilika… lakini tunaamini polisi wanaweza kumruhusu kurudi nyumbani
kupumzika au kuendelea na mahojiano mengine,”alisema Mallya.
Alisema mpaka sasa
anaendelea vizuri na matibabu na afya yake inaendelea kuimarika siku hadi siku
tofauti na alivyokuwa awali. Gwajima alifikishwa polisi kwa madai ya kumtukana
na kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo. Wakati anahojiwa alianguka na kuzimia hali
iliyosababisha akimbizwe katika hospitali ya polisi Kurasini kabla ya
kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na baadaye Hospitali ya
TMJ kwa matibabu zaidi.
Juzi Askofu Gwajima alikwenda polisi akiwa amepandishwa
kwenye baiskeli maalumu ya wagonjwa. Akiwa anainuliwa kwenye kiti na
kupandishwa katika gari, Askofu Gwajima alionekana akikunja uso na kufungua
mdomo kama mtu anayegugumia kutokana na maumivu makali.
Baada ya kutoka
hospitalini msafara huo ulielekea moja kwa moja hadi Kituo cha Polisi cha
Oysterbay na baadaye kuachiwa kwa dhamana
No comments:
Post a Comment