JESHI la polisi mkoani Mara, linamsaka Simion
Otieno,baada ya kudaiwa kuchoma nyumba kwa kutumia mafuta yaa petroli na
kusababisha kifo cha mtoto,Tatu Simion (1).
Tukio hilo lililotokea Machi 31, mwaka huu katika Kijiji
cha Bwai,wilayani Butiama ambapo chanzo chake kinadaiwa ni wivu wa mapenzi kati
ya Otieno na mama wa mtoto huyo, Kudra Janja ambaye ameunguzwa vibaya mwili
mzima.
Janja amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, kwa
matibabu zaidi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mama mdogo wa Janja,Bahati
Magesa, alisema tukio hilo lilitokea nyumbani kwa mjomba wao saa 10 usiku.
Alisema Januari, mwaka huu,mwanaume huyo pamoja na mke
wake walioishi kwa mwaka mmoja,walikuwa na ugomvi kwa muda mrefu.
Alisema Otieno alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa ana
uhusiano wa mapenzi na watu wengine,lakini baadaye ugomvi huo ulikwisha na
waliendelea kuishi vizuri.
“Janja ni mtoto wa dada yangu,mimi naishi mbali kidogo na
kwake,jana usiku (juzi) baada ya tukio, alinisimulia kuwa mume wake aliingia
ndani akiwa na dumu la petroli na alipomuuliza alimwambia alale.
“Baadaye alichukua kiberiti, huku mkewe akimuuliza mbona
unachukua kiberiti usiku huu, akamjibu hayakuhusu, baada ya muda kidogo alitoka
nje, akamwaga mafuta dirishani kisha akawasha moto na kukimbia kusikojulikana,”alisema
Bahati.
Alisema baada ya kuwashwa moto huo,alipiga kelele na
kuomba msaada ndipo mjomba wake Obadia Janja alipomka na kwenda kumsaidia.
“Yaani wakati Obadia anamtoa ndani, tayari alikuwa
ameungua vibaya na mtoto alikuwa ameumia mno,”alisema Bahati.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philip Kalangi
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wameanza kumtafuta muhusika.
Alisema tukio hilo, ni la kinyama na linapaswa kulaaniwa
na kila mmoja na kuiomba jamii kuacha kujichukuliwa sheria mkononi.
No comments:
Post a Comment