Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama
ametoa onyo kwa kikundi cha watu kilichojipanga kumzomea Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe atakayekuwa mgeni rasmi wa Tamasha
la Pasaka
linalotarajiwa kufanyika hii leo katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza na Mwananchi jana, Msama alisema kuwa
amepata taarifa kuhusu uwapo wa mashabiki wa mwanasiasa mmoja, ambao wamenunua tiketi
nyingi kwa lengo la kuzomea.
Msama aliyasema hayo baada ya kuulizwa iwapo alikuwa na
taarifa kuhusu kikundi hicho ambacho kwa mujibu wa habari zilizolifikia gazeti
hili kina lengo la kuingiza watu 1,000 ambacho kimenunua tiketi za Sh5 milioni.
“Hilo suala ninalijua na nimepewa taarifa na baada ya
kuchunguza nikagundua ni kweli, kikundi cha watu kilifika katika kituo cha
kuuzia tiketi cha Mwenge na kuchukua tiketi nyingi na baadaye walikwenda katika
vituo vingine kikiwapo cha Millennium Tower na kununua nyingine,” alisema Msama
na kuongeza:
“Mimi kama mwandaaji nimeamua kuwataarifu maaskofu
mbalimbali ambao ni walezi wangu ili walifahamu hili, pia Katibu wa Umoja wa
Maaskofu ana taarifa hizi, lengo lao tumeshalijua.” Msama ambaye pia ni
Mwenyekiti wa kamati ya tamasha hilo, alisema, “Tumemwalika Membe kwa sababu
hatukutaka kualika mtu ili atupatie fedha au kununuliwa, bali kamati yenye
wachungaji na maaskofu ndiyo iliyoamua yeye awe mgeni rasmi.”
Alisema ifikie hatua dini isitumike kama mwamvuli wa kisiasa.
“Mimi nasema huyo mwanasiasa hagombani na Msama au Membe
bali anagombana na Mungu. Mimi namwachia Mungu haya yote na lazima ajue kwamba
mambo ya kisiasa hayalandani na dini, asiyaingize huku, hili ni tamasha la
kumwabudu Mungu na siyo vinginevyo,” alisema Msama.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste nchini
(CPCT), Askofu David Mwasota alisema mkutano wa Pasaka unaeleweka dunia nzima,
ni siku ya kusherehekea ukombozi hivyo watu wasiutumie tofauti.
“Wote ambao tumewaalika wapo serikalini yaani ni
wafanyakazi wa nchi hii na siyo vinginevyo. Wana hadhi na vigezo kwa kuwa
wameshika nyadhifa kubwa na hilo ndilo tuliloliangalia.
Hatukuangalia vyama na tunachosubiri ni wao kukaa na
kutuletea wagombea, ninachokiona hapa wagombea wataumizana bure, bado hakuna
chama kilichotangaza mgombea, fitina za nini?” alihoji Askofu Mwasota.
No comments:
Post a Comment