MWASISI wa chama cha siasa, Tanzania People’s
Party (TPP), Dk Aleck Che-Mponda (80) amefariki dunia katika hospitali ya
Massana iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na
maradhi ya saratani ya mifupa.
Dk Che-Mponda alikuwa mwanasiasa na msomi wa
sayansi ya siasa na aliwahi kuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Idara wa Sayansi na Utawala mwaka 1980-1991.
Aidha, Dk Che Mponda alifanya utafiti muhimu
kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania kwenye Ziwa Nyasa mwaka
1971. Utafiti huo ulikuwa andiko la Shahada yake ya Udaktari wa Falsafa (PhD),
katika Chuo Kikuu cha Howard, nchini Marekani.
Andiko hilo linaitwa, ‘The Malawi- Tanzania
Border and Territorial Disputes, 1968: A case study of Boundary and Territorial
Imperatives in the new Africa’.
Akizungumzia kifo cha muasisi huyo msomi,
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema alisema kifo cha Dk
Che-Mponda ni pigo kwa wanasiasa na wasomi nchini.
“Tumesikitishwa na kifo cha Dk Che- Mponda,
alikuwa rafiki yetu, tulikua naye kwenye harakati za vyama vya siasa, alianza
vizuri na ari kubwa na pia alikuwa msomi mzuri,” alisema Mrema.
Aliongeza, kifo chake ni majonzi kwani ameondoka
mtu muhimu aliyekuwa mcheshi na mwema kwa wanasiasa wengine na hata katika
jamii.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment