POLISI mkoani Katavi inamshikilia mkazi wa
kitongoji cha Ntumba, kijiji cha Mnyengele wilayani Mpanda, Deogratius Pastory
(30) kwa kumjeruhi vibaya mkewe kwa kumkata mkono wake wa kushoto na kupasua
tumbo la mpenzi wa mkewe kwa panga.
Mtu huyo aliwatendea unyama huo baada ya
kuwafumania mkewe aitwae Tabu Nestory (20) na mpenzi wake wa kiume aitwaye
Masaga Elias (28 wakifanya mapenzi katika jiko la nyumbani kwake kijijini
humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri
Kidavashari alithibitisha mkasa huo. Alisema tukio hilo ni la Machi 23, mwaka
huu saa tano usiku katika kitongoji cha Ntumba katika kijiji cha
Mnyengele.
Akielezea mkasa huo, Kidavashari alidai kuwa
jioni ya siku hiyo ya tukio, mtuhumiwa alimuaga mkewe Tabu kuwa anakwenda
kijiji ambacho kiko umbali mrefu kutoka kijijini hapo kwa ajili ya kuangalia
shamba lao.
Inadaiwa mtuhumiwa huyo alitumia baiskeli yake
katika safari yake hiyo. Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, wakati
mtuhumiwa huyo akiendelea na safari yake ghafla baiskeli yake
aliyokuwa akiitumia katika safari yake hiyo iliharibika, wakati huo ilikuwa
tayari imetimu saa tatu usiku .
“Kwa sababu alikuwa bado amebakiza mwendo mrefu
kufika alikokuwa akienda aliamua kugeuza na kuanza kurejea nyumbani kwake,
ambako alifika saa tano usiku …na alipofika kwake alimkuta mkewe na mpenzi wake
wakifanya mapenzi katika jiko nyumbani kwake,” alieleza.
Inadaiwa kuwa kitendo hicho kilimkasirisha
mtuhumiwa, ambaye alimwamuru mkewe na mgoni wake kuingia ndani, ambapo
alimkamata mwanamume huyo na kumfunga kamba mikononi, kisha akachukua panga na
kumchana tumbo chini ya kitovu hadi utumbo wake ‘ukamwagika’ nje .
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, mtu huyo
alitumia panga hilo alilotumia kuchana tumbo la mgoni wake, kukata mkono wa
kushoto wa mke wake.
Kidavashari alidai kuwa majeruhi wote wawili,
walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda mjini hapa, ambako
wamewalazwa kwa matibabu, ambapo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara tu
upelelezi wa awali wa shauri lake utakapokamilika.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment