WAKILI mwandamizi wa kujitegemea wa jijini hapa, Manase
Keenja (53) mkazi wa Kijenge Mwanama, Arusha, anashikiliwa na jeshi la polisi
kwa tuhuma za kughushi nyaraka za serikali na kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu zaidi ya Sh milioni 320.
Wakili huyo mkongwe mbali ya kujipatia fedha kwa njia
hiyo, pia amekamatwa na mihuri mbalimbali ya serikali, ikiwemo ya Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha, Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kaskazini, mhuri wa ofisi ya Ardhi
Halmashauri ya Jiji la Arusha na mihuri ya Mahakama zote za Mkoa, Wilaya na
mwanzo za Mkoa wa Arusha.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Edward Balele
alipoulizwa juu ya kukamatwa kwa wakili huyo na mwandishi wa gazeti hili
alikiri na kusema kuwa polisi bado inamshikilia kutokana na upelelezi
kutokamilika na upelelezi ukikamilika atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Balele alisema polisi haiwezi kumwachia kwa sasa mpaka
upelelezi utakapokamilika, kwani kuachiwa haraka kunaweza kuharibu upelelezi wa
kesi hiyo.
Alisema kukamatwa kwa wakili Keenja kumetokana na
malalamiko ya wafanyabiashara watatu tofauti wa Jiji la Arusha walioripoti
kituo kikuu cha polisi Arusha juu ya ‘kutapeliwa’ mamilioni ya shilingi na
wakili huyo.
Kamanda huyo alisema miongoni mwa wafanyabiashara
wanaodaiwa kudhulumiwa na wakili huyo ni pamoja na Macklin Temu anayemiliki
kampuni ya maduka ya vipuri vya magari ya Denso, ambaye inaelezwa amepoteza Sh
milioni 120 mbele ya wakili huyo.
Inadaiwa alichukuliwa fedha hizo Aprili 23 mwaka 2013 kwa
kuuziwa kiwanja namba 12 kilichopo katikati ya Jiji la Arusha ambacho
kinamilikiwa na mtanzania mwenye asili ya kiasia Ragieder Kumar, ambaye kwa
sasa ni marehemu kwa kiasi hicho cha fedha.
Kamanda alisema Temu aligundua kutapeliwa Septemba 30
mwaka jana, kuwa hatimiliki ya kiwanja hicho ni ya kughushi na kuripoti kituo
cha polisi Arusha Machi 4 mwaka huu, majira ya saa 7 mchana.
Alisema wakili huyo anatuhumiwa kufanya biashara ya
kitapeli kwa hati hizo hizo za kughushi kwa mfanyabiashara mwingine Valetine
Tarimo (43), mkazi wa Kwa Ngulelo ambaye aliuziwa kiwanja hicho hicho kwa bei
nafuu ya Sh milioni 20.
Kamanda Balele alisema siku chache baada ya Tarimo kutoa
taarifa hiyo, mfanyabiashara mwingine, Jubileth Garson alifika katika kituo
hicho Aprili 25 mwaka huu na kutoa taarifa ya kutapeliwa Sh milioni 182 kwa
hati ile ile feki ya kiwanja namba 12.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment