Hatimaye mwalimu wa chekechea, Mollen Calleb, aliyesimama
mahakamani kwa kujifanya mzazi wa mtoto wa miaka miwili aliyejeruhiwa kwa
kupigwa na mlezi wa shule ya chekechea ya Nelca Day, amehukumiwa kifungo cha
miezi sita jela kwa kosa la kuidanganya mahakama.
Machi 27, mwaka huu, katika Mahakama ya Mwanzo Ilemela,
jijini Mwanza, ilifuta kesi ya kujeruhiwa mwanafunzi, inayomkabili mlezi wa
shule ya chekechea ya Nelca Day Care, Siwema Bujota, anayedaiwa kumpiga mtoto
huyo na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili.
Bujota aliyekuwa na dhamana ya kulea watoto shuleni hapo,
alimjeruhi mwanafunzi wa miaka miwili (jina limehifadhiwa), kwa kumchapa viboko maeneo mbalimbali ya mwili wake kwa
madai kuwa alijisaidia haja kubwa shuleni.
Baada ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani, mwalimu wa
shule hiyo, Calleb alikwenda mahakamani na kujitambulisha kwamba yeye ndiye mlalamikaji wa kesi hiyo na
kuiomba mahakama kuifuta kwa madai kuwa hakuwa na nia ya kuendelea na mashitaka
na kwamba watamalizana nje ya mahakama.Kutokana na maelezo hayo, hakimu
aliyetambulika kwa jina moja la Misana wa mahakama hiyo, alifuta kesi hiyo bila kujua kama huyo
aliyesimama mahakamani si mlalamikaji halali.
Mlalamkaji katika kesi hiyo alikuwa Sabrina Hamis, ambaye
kabla ya kesi kuanza kusikilizwa alikwenda hospitali kwa matibabu ya mtoto
huyo, ambaye hali yake ilibadilika ghafla.
Kufuatia tukio hilo, Hamis alikwenda kutoa taarifa
kituo cha Polisi cha Kilumba, kulalamikia kesi yake kufutwa kinyemela.
Jeshi la polisi mkoani Mwanza lilianza kuwasaka watuhumiwa wote wawili
akiwemo mshtakiwa na mwalimu aliyejifanya mlalamikaji.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Kaimu Kamanda,
Kamishina Msaidizi wa Polisi jijini Mwanza (ACP), Japhet Lusingu, alisema kuwa
Aprili 13, mwaka huu, watuhumiwa hao
walikamatwa.
Alisema Aprili 14, mwaka huu walifikishwa mahakamani na kupata taarifa
kwamba mwalimu huyo amefungwa miezi sita kwa kuidanganya mahakama.
NIPASHE ilizungumza na mlalamikaji ambaye alisema mwalimu
huyo amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kuidanganya mahakama. Aidha,
alisema mtuhumiwa alipelekwa rumande hadi Aprili 23, mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment