Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi
amesema anahofia usalama wa maisha yake,
kufuatia habari iliyoandikwa katika gazeti moja la kila wiki kwamba,
Rais Jakaya Kikwete aliapa kupambana naye jambo ambalo limempa hofu
kubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam, Mengi alisema kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake kuwa yeye ni kinara
wa kuhujumu serikali ya Rais Kikwete siyo za kweli.
Dk.Mengi alisema amesoma kwa masikitiko makubwa habari
iliyochapishwa Machi 23, mwaka huu na gazeti la Taifa Imara, yenye kichwa cha
habari 'Zitto amchongea Mengi kwa JK' ambapo pamoja na mambo mengine inasema
kuwa Zitto Kabwe amemchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete kwamba ndiye kinara wa
kuhujumu serikali yake.
Alisema habari hiyo ambayo chanzo chake kimeelezwa kwamba
ni Ikulu, iliendelea kueleza kuwa Zitto alikutana na Rais Kikwete muda mfupi
baada ya kuwasilisha bungeni ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) kuhusiana na kashfa ya Escrow ambayo Zitto alikuwa ni mwenyekiti wake.
"Habari hiyo inasema kwamba katika mazungumzo yake
na Rais Kikwete Zitto amenukuliwa akimueleza mkuu huyo wa nchi kuwa
anayesababisha serikali yake iyumbe kila mara ni Mengi," alisema Dk.
Mengi.
Dk. Mengi alisema habari hiyo ambayo nakala yake
ameiambatanisha kwenye taarifa yake, inasema yeye Zitto , binafsi amekuwa
akishawishiwa na Dk. Mengi kuiangusha serikali ya Rais Kikwete.
Hata hivyo, Dk. Mengi alisema katika habari hiyo Zitto
alikwenda mbali zaidi kumueleza Rais Kikwete kuwa Dk. Mengi ameapa kuwa Rais
Kikwete akimaliza muda wake wa Urais atamshughulikia kwa nguvu zake zote.
Alisema habari hiyo imeeleza kwamba baada ya maelezo
hayo, Rais Kikwete aliapa kupambana na Dk. Mengi na akamshukuru Zitto kwa kumpa
taarifa hizo.
Mengi alisema tuhuma zilizotolewa kuhusu nia yake ya
kutaka kuiangusha serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza
muda wake wa uongozi, zimemshtua sana na tamko la kwamba Rais Kikwete aliapa
kuwa atapambana na yeye zimempa hofu kuhusu mustakabali wa maisha yake.
Alisema kuwa hofu yake kubwa inasababishwa na Ikulu na
Idara ya habari Maelezo kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi
wowote.
"Najua umakini wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na
Idara ya habari Maelezo katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote
linalomhusu Rais, lakini katika hili nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua
kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa,"alisema Dk. Mengi.
Aliongezea kusema kuwa," hofu yangu inazidi kuwa
kubwa kwa sababu Rais ni Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama. Kauli yake kama
ilivyonukuliwa na gazeti hili kwamba atapambana na mimi inawezekana kuchukuliwa
kama agizo kwa vyombo vya dola kuniangamiza," alisema.
Alitolea mfano mwaka 1170, Askofu Mkuu wa Canterbury
nchini Uingereza aliuawa baada ya walinzi wa mfalme kusikia mfalme akisema
"hakuna anayeweza kuniondolea huyo mkorofi?". Walinzi wake wakadhani
mfalme ameagiza wamuue Askofu huyo na wakamuua, alisema.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment