Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba |
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco),
Felchesmi Mramba, amewahakikishia Watanzania kuwa hakuna mgawo wa umeme.
Wakati Mramba akitangaza hakuna mgawo huo, baadhi ya maeneo yamekuwa yakilalamika
kukatiwa nishati hiyo bila taarifa yoyote ya Tanesco.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam, Mramba alisema Tanesco haijatangaza mgawo wa umeme na kwamba taarifa
iliyotolewa kwenye vyombo vya habari ni kuwapo kwa matengenezo ya kisima cha
Songas ambayo hufanyika kila mwaka.
Alisema mitambo hiyo imeanza kufanyiwa matengenezo tangu
Machi 6, mwaka huu na Shirika lilihakikisha hakutakuwa na athari yoyote kwa
wananchi.
Hata hivyo, alisema Tanesco ina vyanzo vya umeme vya
kujitosheleza katika kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa wateja wake. Mramba alisema hali ya umeme kwa hivi
karibuni imeathiriwa na mvua zilizonyesha kwa mfululizo na kusababisha madhara
katika nguzo za umeme.
Alisema miundombinu ya umeme imeathirika zaidi kwa jijini
la Dar es Salaam kutokana na kuwa
chakavu kwa kuwa imejengwa tangu miaka ya1980 bila kubadilishwa.
Aliongeza kuwa changamoto hiyo imewaletea madhara ingawa
hakusema hasara iliyopatikana na kueleza kuwa bado hawajaijumlisha. “Hakuna
mgawo wa chini chini wala wa juu juu tulihakikisha katika matengenezo ya kisima
hicho cha Songas hapatatokea athari yoyote,” alisema.
Aidha, alisema kuna mitambo mipya ya umeme ambayo
inaendelea kujengwa na kwamba mwishoni mwa mwaka huu kutakuwa na nishati nyingi
kutokana na kukamilika kwa vituo hivyo pamoja na miundombinu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment