Mwishoni mwa wiki iliyopita, wananchi wa Nigeria walipiga
kura kumchagua Rais katika uchaguzi wenye ushindani mkali kati ya Rais wa sasa,
Goodluck Jonathan na mpinzani wake Jenerali Muhamadu Buhari.
Katika makala haya, mtangazaji na mwandaaji wa vipindi katika
idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Salimu Kikeke
anazungumzia uzoefu alioupata katika mchakato wa uchaguzi huo, kama
alivyohojiwa na mwandishi wetu.
Swali: Tueleze uzoefu wako kuhusu matumizi ya mfumo wa
kielektroniki wa kuandikisha wapigakura na pengine changamoto zake ulizozibaini
nchini Nigeria?
Jibu: Nadhani dunia inaelekea katika mfumo wa kidijitali
na itafika wakati pengine kila nchi duniani itakuwa ikitumia mfumo wa
kielektroniki, katika uchaguzi, lakini pia katika mambo mengine mbalimbali.
Kwa kuwa bado ni mfumo mpya, watu wengi hawajaweza
kuelewa hasa unafanyaje kazi. Nadhani uzuri wa mfumo huu, ni kwamba una uwazi
zaidi na matokeo yake yanaweza kuaminiwa na wapiga kura kwa kuwa ni mashine
ambazo hufanya kazi na hilo pia hupunguza uwezekano wa makosa ambayo huweza
kufanywa na binadamu.
Vifaa vya kusomea kadi (card readers) vina betri yenye
uwezo wa kufanya kazi kwa saa 14, na husoma kadi moja kwa chini ya sekunde 60
na ni vigumu ‘kuchakachua’ labda mtu aghushi ‘VIN,’ yaani namba maalumu ya mpigakura.
Kwa hiyo mfumo huu una ufanisi mkubwa, lakini kama
teknolojia nyingine zozote mpya, zina changamoto zake siku za mwanzo, na
zinapozoeleka hali inakuwa tofauti.
Swali: Kipi kimekukosha na kukusononesha kuhusu mchakato
mzima wa uandikishaji na uendeshwaji wa kampeni nchini Nigeria?
Jibu: Hii ni moja ya nchi zinazoelezwa kuwa na demokrasia
kubwa barani Afrika. Pia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi,
uchaguzi huu una ushindani mkali kati ya wagombea urais ambao ni Goodluck
Jonathan wa chama tawala PDP na Jenerali Muhhamadu Buhari wa chama cha upinzani
APC, wanavutana vikali kabisa.
Kitu ambacho kimenivutia hasa ninapozungumza na wananchi
wa hapa, ni kutaja suala la amani. Licha ya vuta nikuvute iliyopo, wengi
wanasema cha msingi ni kufanya uchaguzi huu kwa amani. Kumekuwa na vijembe vya
hapa na pale, na wakati mwingine ghadhabu ambazo unaweza kudhani zitavuka
mipaka na kuleta tafrani, lakini hilo halijajitokeza kwa kiwango kikubwa cha
kutisha- ukiacha matukio ya Desemba mwaka jana, ambapo kwa mujibu wa Tume ya
Taifa ya haki za Binadamu watu takriban 58 waliuawa katika ghasia zinazihusiana
na uchaguzi katika sehemu mbalimbali.
Pamoja na kuwa masuala makuu kama usalama, ufisadi na
uchumi ni mambo yanayozungumzwa zaidi kwenye vyombo vya habari, wananchi wengi
wa kawaida wanataka mambo ya kila siku maishani kama vile umeme na maji, lakini
kubwa kuliko yote wanataka amani.
Kampeni kwa jumla zimekuwa salama na kwa kuwa kuna
ushindani mkali katika urais, wagombea wamekuwa wakijinadi kwa kusema
kinagaubaga jinsi watakavyokabiliana na changamoto za taifa hili. JaSwali: Tume
ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), imekuwa ikilalamikiwa kwa kutokuwa chombo huru,
hali ikoje Nigeria kuhusu chombo kinachosimamia masuala ya uchaguzi?
Jibu: Hii ni changamoto kubwa kwa Mwenyekiti wa Tume huru
ya Uchaguzi ya Taifa ya Nigeria (INEC). Profesa Attahiru Muhammadu Jega
aliteuliwa na Rais Goodluck Jonathan kuongoza taasisi hii muhimu Juni 8 mwaka
2010, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti Profesa Maurice .
Kuteuliwa kwake kuliidhinishwa na mkutano wa vigogo
uliohudhuriwa na viongozi wa zamani wanaoheshimika kama vile Yakubu Gowon,
Muhammadu Buhari (Mgombea wa upinzani wa sasa), Ibrahim Babangida, Abdulsalami
Abubakar, Ernest Shonekan, Olusegun Obasanjo na Shehu Shagari.
Wengi kutoka vyama vya kiraia na hata wanasiasa
waliupokea vyema uteuzi huo na wananchi wana imani kuwa Profesa Jega ataweza
kazi hii na ataifanya kwa uhuru na uwazi.
Nigeria ikitajwa kuwa na demokrasia kubwa Afrika
haitotaka kuharibu jina lake, hasa kwa kutazama nchi jirani ya Ghana ambayo
Mwenyekiti wake, Kwadwo Afari-Gyan ameshikiliwa wadhifa huo tangu mwaka 1993.
Wadadisi wanasema Jega naye anaweza kufanya hivyo kama atapatiwa nafasi.
Swali: Ukiwa Mtanzania unafahamu fika taratibu za mfumo
wa uchaguzi uliopo nyumbani, Je, mfumo huu una tofauti yoyote na unaotumika
Nigeria?
Jibu: Mifumo inafanana kwenye uchaguzi wa urais na
wabunge. Kuna wagombea urais 14, lakini wawili ndio wanachuana zaidi ambao ni
Goodluck Jonathan na Muhammadu Buhari. Kura ni ya siri kama Tanzania na rais
anapigiwa kura na wananchi, na anayepata kura nyingi zaidi ndio anakuwa
mshindi. Tofauti na Tanzania huku kuna mfumo wa magavana ambao uchaguzi wao
unatarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Swali: Unautazamaje ushiriki wa vyombo vya habari katika
mchakato wa uchaguzi huko, Je, kuna mazingira mwafaka na huru kwa vyombo
kufuatilia uchaguzi?
Jibu: Kihistoria ukitazama, Nigeria imekuwa na uhuru
mkubwa wa habari pengine kuliko nchi yeyote ile barani Afrika.
Pamoja na kuwa katika miaka ya nyuma wamepitia changamoto
kubwa hasa katika enzi za utawala wa kijeshi, lakini vyombo vya habari, hasa
magazeti yameweza kukabiliana vilivyo na changamoto hizo.
Katika uchaguzi huu, ambao una mvutano mkali katika
nafasi ya urais, wananchi wanapata nafasi ya kusoma yote; mabaya na mazuri ya
wagombea na hivyo kuwapa wapiga kura taswira ya kile wanachotaka inapofika siku
ya upigaji kura.mbo zuri pengine ni kuwa wote wamewahi kuongoza taifa hili.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment