TAASISI za dini ziko hatarini kufutwa katika orodha ya
usajili kutokana na kuvunja sheria kwa kushindwa kutoa taarifa za mapato na
matumizi ya hesabu za fedha kwa mwaka, imeelezwa.
Kazi ya kuzifuta taasisi hizo, inatarajia kufanyika Jumatatu ijayo, baada ya
kukamilisha uchambuzi
wa taasisi hizo na kwamba itaanzia jijini Dar es Salaam
na baaadaye mikoani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe,
alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,
kuhusu mustakabali wa nchi.
Alisema taasisi hizo ni zile ambazo hazifuati matakwa ya
kisheria ikiwemo kuwasilisha taarifa za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa
ada.
Chikawe alisema baadhi ya taasisi hizo ambazo zinakiuka
sheria pia katika siku za hivi karibuni viongozi wa taasisi hizo, wamekuwa wakitoa
matamko yanayoashiria kuingilia masuala ya kisiasa, kinyume cha sheria na
katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.
Waziri Chikawe alisema matukio hayo yamekuwa
yakisababishwa na hamasa za kisiasa au baadhi ya watu waliokuwa wakitumia muda
huo kutekeleza ajenda zao kwa kisingizio cha vuguvugu za kisiasa.
Alisema viongozi wa taasisi hizo wana haki ya kushiriki
katika masuala ya kisiasa kama watu binafsi lakini ni kinyume cha sheria Sura
ya 337, kutumia uongozi wao kushawishi waumini kutekeleza matakwa yao ya
kisiasa.
Waziri alisema baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakitoa
matamshi ya kulenga na kushawishi wafuasi wao wafuate maelekezo yao kuhusiana
na masuala ya Katiba Inayopendekezwa au kuhusu uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
“Matamshi haya yanakiuka sheria za usajili wa taasisi
hizo na hivyo serikali inatoa onyo kali kwa vikundi, zikiwemo taasisi hizo
kuepuka kushiriki katika vitendo ambavyo vinaashiria kuvuruga amani na utulivu
nchini,” alisema.
Pia katika mkutano huo, Chikawe alizungumzia suala la
viongozi wa dini wanapochangisha pesa na kuandamana au kukutana na wanasiasa
kwa kile kinachodaiwa kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
“Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni huku katiba
zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizi zinaeleza wazi kuwa kitendo hicho si
kazi ya taasisi hizo,” alisema.
Alisema kuendelea kwa matukio hayo ya taasisi hizo
kushiriki katika mambo ya kisiasa kunaashiria kuvurugika kwa amani na utulivu
wa nchi.
Alisema matukio hayo yanahashiria uvunjifu wa amani na utulivu
na kwamba lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha taasisi hizo pamoja na
viongozi wake wanadhibitiwa.
Wiki iliyopita,Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima, alihojiwa kwa
takribani saa sita katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam.
Gwajima alihojiwa kwa tuhuma za kutoa maneno ya kashfa na
matusi kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp
Kardinali Pengo, Februari, mwaka huu.
Kabla ya kufikishwa Kituo cha kati, alihojiwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay wiki mbili
baada ya kuzirai akiwa kwenye kituo kikuu cha polisi na kupelekwa katika
hospitali ya TMJ, Mikocheni kwa ajili ya matibabu.
Mbali na kumhoji, polisi walimtaka kuwasilisha orodha ya
mali zake, fedha alizo nazo katika benki tofauti, hati ya kumiliki helkopta,
makanisa yake yote na ndugu zake walio hai na walio kufa.
Gwajima alitakiwa
kurudi tena kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, kesho.
UHURUONLINE
No comments:
Post a Comment