Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Dk Fadhili Kibaya
ambaye ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Maweni amesema, Tukio
hilo limetokea leo majira ya saa saba ambapo alipokea majeruhi 15 na miili 8
ikiwemo 6 ya wanafunzi, mwalimu mmoja wa shule ya msingi Kibilizi na mkazi
mmoja wa Bangwe.
Dk. Kibaya amewataja marehemu hao kuwa ni Focus
Ntahaba(35), Elieza Mbwambo mwalimu (25) Yusuph Athumani (8), Hassani Ally (9),
Fatuma Sley (7), Zamda Sefu (8), Shukrani Yohana (7) na Walupe Kapupa (10) wote
wanafunzi wa shule ya Msingi Kibirizi.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni Mwalimu wa darasa la
kwanza shuleni hapo, Melina Sililo
amesema, wakati alipokuwa akiendelea na kufundisha aliona wingu likitanda na
Mvua ikaanza kunyesha jambo lililosababisha giza.
Amesema hali hiyo ilimfanya ashindwe kufundisha na wakati
huohuo radi zilipigwa na moto ukatanda darasa zima ambapo yeye pamoja na
watoto zaidi ya kumi walianguka.
“ Nilipata ufahamu na nikajikokota ofisi ya mwalimu mkuu
kuomba msaada, tukawabeba wanafunzi na kuwapeleka ofisi ya mwalimu mkuu,
tulijaribu kuwapa huduma ya kwanza kwa kuwapaka chumvi bahati mbaya katika hao
nane wanafunzi sita wakawa tayari wamefariki” Asema Mwalimu Sililo.
Aidha amesema mwalimu Mbwambo alizimia kwa muda kidogo na
baada ya kuhangaika kumpatia msaada walimkuta amekwisha fariki hali
iliyowalazimu kuomba msaada wa gari la kuwafikisha maiti hao pamoja na majeruhi
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Maweni.
Pamoja na hayo majirani wa shule hiyo ambao ni James
Leonard na Rucia Mathiasi wameeleza kusikitisha na tukio hilo ambapo walisema
matukio hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hasa wakati wa Mvua na kwamba
mara nyingi yamekuwa yakihusishwa na imani za Kishirikina.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment