Siku moja baada ya Bunge kupitisha muswada wa Sheria ya
Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kasi ya matumizi mabaya ya mitandao ikihusisha
majina ya wabunge imeendelea.
Jumatano wiki hii, Bunge lilipitisha muswada huo
wenye
vifungu 59 vya sheria baada ya kukaa zaidi ya saa saba ili kupitia kifungu hadi
kifungu.
Licha ya Muswada huo wa sheria kupitishwa, baadhi ya watu
wameendelea kutumia mitandao ya kijamii kinyume cha sheria kwa kufungua
akaunti/ kuingilia zile zilizofunguliwa na viongozi na kutuma jumbe za
kuwalaghai au kuwahadaa wananchi bila kujali kuwa kitendo hicho ni kinyume cha
sheria.
Gazeti la NIPASHE lilibaini akaunti ya David Kafulila
aliyoifungua mtandao wa Facebook, ikiwa imeandikwa: 'Habari za asubuhi ndugu
wananchi, natumai wengi wetu tumeiona siku ya leo ya Alhamisi na nina imani
kila mmoja wenu ameamka na afya njema....Ndugu wananchi naomba tuchangie mawazo
kwa moyo mmoja kupitia mada hii na iwapo nitapendezwa na wazo la Mtanzania
yeyote bila kujali itikadi yoyote naahidi kumuwezesha.
Mada ni hii: KWA MTAJI WA TSHS MIL.15 NI SHUGHULI GANI
UNAWEZA KUIFANYA IKAKUWEZESHA KUKUIMARISHA UCHUMI WAKO BILA KUPATA HASARA
ITAYOPELEKEA KUMALIZA HADI MTAJI HUU WA TSHS MIL.15.
Naomba tuchangie mawazo kwa pamoja ndugu wananchi huwezi
jua iwapo wazo lako litakuwa zuri litakupa nafasi nikakuwezesha kupitia wazo
lako hilo.
HIZI NDIO FURSA ZENYE /SHARE NA MTANZANIA MWENZAKO AJE
KUCHANGIA" mwisho wa kunukuu.
Baada ya mwandishi wa habari hizi kusoma ukurasa huo,
aliwasiliana na mbunge huyo, ambaye alikanusha kuandika kwenye ukurasa huo.
Kafulila alisema maelezo hayo siyo yake na kueleza kuwa
watu hao ni matapeli ambao wamekuwa wakiingilia mitandao ya viongozi
kurubuni/kuwadanganya wananchi.
Akitoa maoni yake kuhusiana na vitendo hivyo, alisema
lazima kuwapo kwa mfumo utakaosaidia namna ya kumpata mtu anayetumia jina la
mwingine au jina feki kufanya utapeli.
"Uhuni huu wa kuingilia akaunti yangu ya Facebook
umenisumbua kwa muda mrefu na kunikosesha amani mimi binafsi na wadau wa
mtandao ambao nimekuwa nikiwasiliana nao kwa njia ya mtandao," alisema.
Wabunge wengine ambao wamekumbwa na karaha hiyo ni pamoja
na aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye jina lake
lilitumika kwenye mtandao huo kuwarubuni Watanzania.
Mbunge mwingine ambaye jina lake liliwahi kutumika vibaya
kwenye mtandao huo ni la Halima Mdee (mbunge wa Kawe), ambaye mara ya mwisho,
ukurasa wenye jina lake kuliandikwa kuwa
Mdee ameanzisha Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccoss) wakati sio kweli.
No comments:
Post a Comment