KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA, DAVID MSIME |
Jeshi la Polisi mkoani hapa limefunga vituo vitatu katika
eneo la Nkuhungu baada ya kubaini uwepo wa watoto na vijana 115 kutoka mikoa
13, ikiwa ni pamoja na visiwani Zanzibar, waliokuwa wakilelewa kwenye mazingira
hatarishi.
Hata hivyo, kubainika kwa watoto hao ni tofauti na
matukio ya mkoani Kilimanjaro ambako Jeshi la Polisi lilibaini zaidi ya watoto
200 waliokuwa wamefungiwa kwa miaka takriban mitatu wakipewa mafunzo ya kisiri
na hivyo kuibua hisia za ugaidi.
Katika tukio la Dodoma, polisi imesema inaendelea na
uchunguzi kujua walichokuwa wakifundishwa vijana hao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,
kamanda wa polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema watoto hao wanatoka
katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara, Kagera, Tanga,
Tabora, Singida, Pwani, Lindi, Geita, Mwanza na Manyara.
Alisema baada ya kupokea taarifa ya uwepo wa watoto hao,
walifika katika vituo hivyo saa 6:30 usiku jana na kukuta watoto hao wenye umri
wa chini ya miaka 25.
“Polisi iligundua vituo vitatu katika eneo la Nkuhungu,
Dodoma Mjini baada ya kupokea taarifa kwamba kuna nyumba ambazo zinaonekana
kuingia watoto wengi na inawezekana siyo mazingira salama ya kuishi binadamu
hasa watoto na wanachofundishwa huenda ni kinyume cha maadili,” alisema.
Kamanda Msime alisema katika vituo hivyo walipatikana
jumla ya watoto 63 wenye umri wa chini ya miaka 18, wakati walio na vijana
wenye umri wa kati ya miaka 18 na 25 walikuwa ni 52. Alifafanua kuwa kati ya watoto
hao waliotoka Wilaya ya Kondoa mkoani hapa ni 50 wakati waliotoka wilaya za
Dodoma Mjini, Chamwino na Mpwapwa ni watoto 26.
“Uchunguzi unaendelea na yeyote atakayeguswa na ushahidi
kuwa amekiuka sheria atafikishwa mahakamani, wakiwemo wazazi walioruhusu watoto
kuwa katika uangalizi ambao siyo wa kutosha kama sheria ya watoto ya mwaka 2009
inavyoelekeza,” alisema.
Pia alisema jeshi hilo linachunguza watoto hao walikuwa
wakifundishwa kitu gani na kama walikuwa wakihudhuria shule kulingana na umri
wao na sheria za nchi zinavyoelekezwa.
Ingawa hakulihusisha tukio hilo na mafunzo ya ugaidi,
Kamanda Misime aliwataka viongozi na watu wataka maeneo kama hayo katika himaya
zao na vituo visivyosajiliwa ambavyo ni hatarishi kwa watoto, watoe taarifa
mapema.
Pia alitoa wito kwa familia, viongozi wa serikali za
mitaa, dini na taasisi nyingine kutoruhusu watoto wao kupelekwa na kuelelewa
katika vituo hatarishi.
Aidha, aliwataka wazazi wanaofahamu watoto hao wajitokeze
ili kupewa maelekezo kabla ya kutafutwa na mkono wa dola.
Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini, ambaye ni mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama, Betty Mkwasa alisema jana kuwa aliyoyaona katika
kituo hicho hayakubaliki.
“Kwanza watoto wanalala wengi, hakuna hewa ya kutosha,
wanajipikia wenyewe chakula na hawana uangalizi wa watu wazima,” alisema
Mkwasa.
Alisema serikali haikatai dini yoyote kufundishwa kwa
watoto bali taratibu, kanuni, sheria pamoja na haki za mtoto lazima zifuatwe.
“Siwezi kujua walikuwa wanafundishwa nini lakini baada ya
upembuzi yakinifu utakaofanywa na wataalam ambao nimekuja nao, tutaweza
kuzungumza kama walifuata kanuni na utaratibu,” alisema.
Mwananchi ilipofika katika moja ya kituo hicho, jana
asubuhi lilikuta watoto hao wakicheza kwenye eneo hilo lililokuwa chini ya
ulinzi wa polisi waliokuwa na silaha za moto.
Watoto wengi walikuwa hawajavaa viatu na baadhi yao
walisema kuwa viatu walivyokuja navyo kutoka makwao vimeshakwisha.
Bakwata
Sheikh mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Shaaban Rajabu
alisema wanakitambua kituo hicho kama ilivyo kwa vituo vingine vinavyofundisha
dini ya Kiislamu.
Sheikh huyo alipinga suala la watoto kukosa elimu,
akisema wazazi wao wamehiyari vijana wao kusoma dini tu.
“Naomba ifahamike kuwa, wapo wazazi ambao wanapenda
watoto wao wasome dini tu na hata mimi nilisoma hivyo kabla ya kwenda nje kwa
masomo zaidi na kurudi,” alisema.
Alipinga suala la kusajiliwa kwa kituo akisema viko vituo
vingi havijasajiliwa hata katika dini nyingine, lakini havisumbuliwi na
kushangazwa kuona utaratibu wao unakuwa na shida.
Kwa upande mwingine alishauri Bunge kutunga sheria kali
kwa ajili ya kuvilazimisha vituo vyote kuwa na usajili ili viweze kufuatiliwa
kulingana na matakwa ya serikali.
Kwa upande wake, katibu wa Bakwata mkoani hapa, Hassan
Kuzungu, aliyeongozana na kamati hiyo, alieleza kusikitishwa na kitendo cha
mazingira waliyokuwapo watoto hao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nkhungu, Kasian Mponela alisema
kuwa amekuwa akiwaona watoto hao, lakini hajui wanachojifunza hapo.
Alisema suala la kuangalia kama wanajifunza dini au mambo
mengine sio jukumu lake, kwani yeye anajua kila mtu anapanga mwenyewe matumizi
ya nyumba yake.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment