Friday, April 17, 2015

Polisi wamfuata Askofu Gwajima nyumbani kwake kumchukua kumpeleka Central...Askofu hakuwa tayari badala yake akajisalimisha kwa Kova akiwa na wakili wake

Waumini waliotanda nje ya nyumba ya Gwajima
Askofu Gwajima ‘aidindia’ jeshi la Polisi waliomfuata kumchukua nyumbani kwake SalaSala, ajisalimisha na Wakili wake kwa Kamanda Kova.

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima  mapema leo ameibua hofu kubwa  kwa majirani  na waumini wake waliokuwa wametanda nje ya nyumba yake
baada ya Jeshi la Polisi kuvamia kwake kwa lengo la kumchukua kwenda Polisi Centro (Makao maalum yaa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam).

Mbilinge hilo lililoanza majira ya saa 12, asubuhi kufuatia magari ya Polisi matatu kufika kwake na kumtaka wamchukue, hata hivyo Askofu Gwajima hakuwa tayari kufungua mlango wala kutoa ushirikiano hali iliyozua taaruki kwa majirani.

Kwa mujibu wa mashuhuda walioshuhudia tukio hilo, walieleza kuwa, baada ya kuona magari ya Polisi yaamepaki nje ya nyumba ya Askofu Gwajima, walianza kupatwa na wasiwasi hali iliyozua fununu huenda kuna jambo baya limetokea.

Mmoja wa majirani hao ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake, alibainisha kuwa, baada ya kuona gari za Polisi zipo nje ya nyumba ya Gwajima alisogea kwa lengo la kutaka kujua kulikoni ndipo alipobaini kuwa Polisi hao walikuwa wanamtaka Gwajima ambaye hata hivyo alikuwa ndani pasipo kufungua geti la nyumba yake.

“Nilisogea kuhoji kwa jirani yangu lakini nilipoona Polisi ilibidi nirudi. Lakini baada ya muda waumini wake nao walianza kukusanyika na kukaa nje ya nyumba yake” alieleza jirani huyo, majira ya saa mbili asubuhi.


Mtumshi wa Mungu Mtume Dk. Vernon Ferdnandes wa AGAPE, akiwa eneo la tukio akiwa ameungana na maaskofu wengine waliofika kuungana na mwenzao Askofu Gwajima.

Hata hivyo, Moblog iliyokuwa eneo la tukio hilo kuanzia majira ya saa moja asubuhi, ilianza kushuhudia umati mkubwa wa waumini wa Askofu Gwajima ukisogea eneo hilo la nyumba yake na kutanda nje ya geti.

Waumini hao walipofika hawakuwa tayari kuongea na mtu yoyote hapo nje zaidi wao kwa wao walionekana kuonyeshana ishara maalum huku wakijaribu kufuatilia mienendo ya Polisi hao ambao walifika na magari zaidi ya matatu, huku magari hayo matatu ikiwemo Suzuki, Land cruiser namba T337AK na Pick up aina ya Ford namba PT 288, yaliyoonekana hapo ambapo walikuwa wakifanya mawasiliano yao.

Picha iliyopigwa mapema na Modewji blog, kabla ya wafuasi wa Askofu Gwajima hawajaanza kufika, ilionyesha gari la Polisi likionekana kuweka doria huku magari mengine yanayoonekana kwa mbele ya gari hilo ni ya maafisa wa Polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kawaida.

Kadri muda ulivyozidi kwendelea ndipo waumini wa Askofu Gwajima walikuwa wakiongezeka kwenye eneo hilo, ambaapo majira ya saa sita mchana magari hayo ya jeshi la Polisi yaliondoka nyumbani kwa Askofu Gwajima moja moja, huku waumini hao wakiendelea kufuatilia mwenendo  wa kila aliyesogea eneo la nyumba hiyo ambayo pia wandishi wa habari tuliokuwa hapo nje.

Baadhi ya waumini walieleza kuwa,  wakati wakiwa katika kujiandaa na maombi pale Kawe wanapokuwa na maombi yao ya kila Ijumaa na Jumamosi ambayo kabla ya Ibada, walishangaa kutomuona Askofu Gwajima kufika kwenye eneo hilo la Kawe, ndipo walipopatwa na wasiwasi na walipowasiliana naye, ndipo walipoamua wote kwa pamoja kutoka Kawe kwenda Sala Sala kwa lengo la kushuhudia kulikoni na kukuta jeshi hilo la Polisi likiwa limezingira nyumba hiyo kwa lengo la kumchukua.

Hata hivyo, vyanzo mbalimbali vya ‘Kiintelijensia’ vilieleza kuwa, Jeshi hilo lilipoona umaati wa waumini wa Askofu Gwajima kuongezeka kila wakati, waliamua kuwasiliana na viongozi wao wa juu na ndipo walipoamua kuondoka.



Wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatara akiongea machache kwa wandisshi wa habari dhidi ya Mteja wake, muda mfupi baada ya kutoka nje ya nyumba ya Gwajima

Wakili wa Gwajima anena.
Hata hivyo baada ya mashauriano ya muda mrefu, Askofu Gwajima aliweza kutoka huku akiwa ndani ya gari  lenye namba T 159 DDH, akiwa amekaa nyuma na walinzi wake wa Usalama wawili waliovalia makoti na miwani meusi, ambapo Wakili Peter Kibatala aliweza kukaa mbele huku akisisitiza kutoongea lolote kwa mteja wake.

Baada ya kutoka gari hilo nje  ya geti, waumini wake hao walikuwa wakiita Baba! Baba! Baba!, kwa lengo la kutaka kumuona na kumpa mkono, lakini ilishindikana huku Wakili wake akisisitiza kuwa mteja wake hatokuwa tayari kuongea na wandishi wa habari, lakini baada ya kubanwa na wandishi wa habari, Kibatara aliweza kuongea machache!.

“Tunaelekea Polisi central makao makuu kuutikia wito wa jeshi la Polisi waliofika hapa tokea alfajiri. Hivyo baada ya hapo ndipo tutaongea na wandishi wa habari.  Mambo yote ni ya kisheria hivyo baada ya wito kukubali ndipo tutatoa taarifa hichi ndipo tulichokubaliana” alieleza Wakili Kibatara.

Hata hivyo baada ya kuongea na wandishi wa habari, gari hilo lilitoka eneo hilo kwa mwendo kasi huku magari mengine ya maaskofu nao yakiunga kwa mwendo kasi yakimsindikiza.




Wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatara akiondoka eneo la nyumba ya Gwajima huku Askofu Gwajima akiwa ndani ya gari hilo kwa nyuma.


Mwandishi Mwandamizi wa mtandao wa Modewji blog, Andrew Chale alikuwa eneo la tukio nyumbani kwa Askofu Gwajima, eneo la SalaSala, ambaye alipiga kambi kuanzia asubuhi ya leo hadi majira ya mchana wa saa nane baada ya Askofu Gwajima, kutii amri ya kukubali wito wa kwenda Polisi Central
CHANZO: MO DEWJI BLOG

No comments:

Post a Comment