Maaskofu na Wachungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima
linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima (pichani), waliokamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutaka
kumtorosha kiongozi huyo, kutoka hospitali ya TMJ, wanatarajia kufungua kesi
mahakamani.
Wafuasi hao wapatao 15 waliokamatwa na
Jeshi la
Polisi Machi 29, mwaka huu usiku wakituhumiwa
kutaka kumtorosha Askofu Gwajima wanatarajia kufungua kesi ya kikatiba katika
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Jeshi la Polisi.
Wakili wa utetezi wa Askofu Gwajima na Kanisa la Ufufuo
na Uzima, Peter Kibatala, alisema jana kuwa
wachungaji na viongozi hao
waandamizi wamepanga kufungua kesi kulalamikia namna walivyotendewa na Jeshi la
Polisi walipokamatwa.
Alisema wamepanga kufungua kesi hiyo kuanzia leo kwa
lengo la kudai haki ya kuonewa kwa watumishi hao.
Kibatala alieleza kuwa mkutano na waandishi wa habari
ulioitishwa na Kamanada wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova, ulikuwa na mahudhui ya kuwahukumu viongozi hao waandamizi kama wahalifu
wakati walikuwa hawakuwa wameshtakiwa na chombo chochote.
“Press conference (mkutano wa waandishi wa habari)
unapaswa kuendeshwa kwa namna ambayo haimhukumu mtu moja kwa moja, lakini
Kamanda Kova aliendesha mkutano ule kwa kuwahukumu moja kwa moja,” alisema
Kibatala.
Madai mengine ni wafuasi hao kukaa polisi muda mrefu
kuliko muda uliowekwa na sheria bila kufikishwa mahakamani.
Lingine ni miongoni wa Maaskofu na wachungaji hao, wawili
waliteswa na maofisa wawili wa Jeshi la Polisi wakati wanahojiwa.
Alisema kutokana na mambo hayo matatu, viongozi hao
wanalalamika kuwa yamevunja haki yao ya kikatiba.
Aliongeza kuwa hata barua aliyowaandikia Jeshi la Polisi
juzi kutaka Askofu Gwajima kutofika kituo cha polisi hadi pale watakapopata
nyaraka ya kisheri kutoka kwa Jeshi hilo, pia ilielezea matarajio ya kufungua
kesi mahakamani juu ya malalamiko ya viongozi hao.
Kibatala alivitaja vitu walivyorudishiwa viongozi hao ni
pamoja na magari matatu pamoja na vifaa
vya matangazo walivyonyang’anywa na Jeshi la polisi.
“Kwa hiyo leo (jana) wafuasi hao wameambiwa wasiende
kuripoti polisi hadi pale watakapotaarifiwa na Jeshi la Polisi,” alisema
Kibatala.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment